Na. Faustine Kapama-Mahakama, Lushoto
Ziara
ya Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo imengia siku ya pili
ambapo leo tarehe 25 Mei 2022 ametembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) na kupokelewa na mwenyeji wake, Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Paul Kihwelo.
Akiwa
chuoni hapo, Mhe. Owiny-Dollo alipitishwa katika maeneno mbalimbali, ikiwemo ofisi
kadhaa, vyumba vya madarasa, Maktaba iliyosheheni vitabu mbalimbali na kwenye
mabweni ya wanafunzi. Jaji Mkuu huyo pia alijionea jengo jipya la kisasa ambalo
mara litakapokamilika litatumiwa na wavulana.
Katika
moja ya vyumba vya madarasa alivyotembelea alikuta wanafunzi wakiendelea na
masomo na kuwahimiza kusoma kwa bidii ili waweze kufanikiwa katika mipango yao
ambayo wamejiwekea katika maisha.
Baadaye
alipanda mti katika moja ya maeneo ya chuo hicho kama kumbukumbu ya ujio wake
kabla ya kushiriki kwenye kipindi maalumu kilichokuwa kimeandaliwa kwa lengo la
kubadilishana uzoefu wa namna ya kuendesha vyuo vya Mahakama, hatua
itakayosaidia kuiwezesha Mahakama ya Uganda kujifunza jinsi ya kuijengea uwezo
Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama nchini Uganda (JTI).
Mhe.
Owiny-Dollo, ambaye ameambatana na ujumbe wa maafisa 12 kutoka nchini Uganda alisema
kuwa wamekuja nchini Tanzania kupata maarifa na wanatumaini kujifunza mengi
kutoka katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na pia kupata uelewa
jinsi ya kuijengea uwezo wa Taasisi yao.
Akieleza
kwa ufupi historia ya chuo hicho, Mhe. Kihwelo alisema kuwa hadi miaka ya 1970,
ardhi ilikuwa inamilikiwa na Bw. Ernest Smith na ilitumiwa kwa shughuli za
shule za awali za watoto wadogo wa Kiingereza. Baadaye ardhi hiyo iliuzwa kwa
Shirika la Wamisionari wa Romani Katoliki, yaani Baraza la Maaskofu Tanzania
(TEC) ambao baadaye waliikabidhi kwa Serikali.
Aliwaeleza
wageni hao kuwa Serikali ilitumia eneo hilo kama Kituo cha Mafunzo Vijijini
hadi 1974 na mwaka huo wa 1974, Serikali ilikabidhi ardhi hiyo kwa chama tawala
wakati huo, TANU, ambao waliamua kukitumia kama chuo cha masuala ya itikadi.
Kwa
mujibu wa Mhe. Kihwelo, mwaka 1992 mazungumzo yalianza kati ya Serikali na
chama tawala juu ya uwezekano wa kuandaa taasisi ya mafunzo ya Mahakama katika
majengo ya sasa, ambapo tarehe 30 Desemba, 1992 chama tawala kilisalimisha
ardhi hiyo kwa Serikali na kisha kukabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania Februari
1993.
“Chuo cha IJA kilianzishwa kwa Sheria ya
Bunge, Sheria Namba 3 ya 1998. Kilianza kazi yake tarehe 23 Oktoba, 2000 na
kilikuwa kinatoa Cheti na Diploma ya Kozi za Sheria. Uzinduzi rasmi ulifanywa
na Rais Benjamin Mkapa tarehe 3 Agosti 2001,” alisema.
Mkuu
wa Chuo huyo alitaja baadhi ya kazi za IJA kuwa ni kuendelea na elimu ya Mahakama
na sheria, masomo ya sheria, utafiti wa kimahakama, ushauri, kutoa mafunzo kwa mawakili
wapya walioajiriwa katika sekta za umma na wanaowania Udalali wa Mahakama na Wasambaza
Nyaraka.
Awali,
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika aliwakaribisha wageni hao katika Chuo
cha IJA ambapo alielezea furaha yake kwa kupata
ugeni huo wa Jaji Mkuu kutoka Uganda ulioambatana na ujumbe mzito. Alisema kuwa
kukutana kwao ni fursa muhimu watakayoitumia kujifunza mambo mbalimbali, kubadilishana
uzoefu jinsi vyuo vyao vya Mahakama vinavyofanya kazi.
Miongoni
mwa viongozi walioambatana na Jaji Mkuu wa Uganda ni Jaji Kiongozi wa Uganda, Dkt.
Flavian Zeija, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Mhe. Sarah Langa Siu, Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya JTI Uganda, Mhe. Damilie Lwanga, Msajili wa Taasisi ya
JTI Uganda, Mhe. Moses Angualia na
viongozi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria Uganda (IDLO).
Ziara
hiyo ni sehemu ya ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya
Uganda na ujirani mwema kati ya nchi hizi mbili.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Dkt. Ubena Agatho akisalimiana na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo.
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo akizungumza na baadhi ya Mahakimu Wakazi kutoka katika Mahakama ya Wilaya Lushoto walioshiriki katika mapokezi yake.
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Mkuu wa Chuo cha IJA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni