Na. Faustine Kapama, Mahakama, Tanga.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema sensa ya watu na anuani
za makazi inayoratibiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaisaidia
Mahakama ya Tanzania kupanga upya mpango wa ujenzi wa miundombinu, ikiwemo
ujenzi wa Mahakama mbalimbali hapa nchini.
Mhe.
Prof. Juma ameyasema hayo leo tarehe 18 Mei, 2022 katika siku ya tatu ya ziara
yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga alipokuwa akizungumza na Mkuu wa
Wilaya ya Lushoto, Mhe. Kalisti Lazaro ofisini kwake. Katika mazungumzo hayo,
Jaji Mkuu ameainisha vipaumbele vinne, ikiwemo idadi
ya watu na wingi wa mashauri, vinavyotumiwa na Mahakama ya Tanzania kubaini
maeneo ya ujenzi wa miundombinu, hususani Mahakama za Mwanzo na Wilaya.
“Kama mnavyofahamu mwaka huu tutakuwa na sensa
ya watu. Kwetu kama Mahakama ni zoezi muhimu sana kwa sababu linatupa mahesabu
mapya ya watu na maeneo mbalimbali ambayo yanahitaji huduma. Lengo la sensa ni
kusogeza huduma, hivyo tutasubiri matokeo
hayo ya sensa ili yatusaidie katika Mkoa huu wa Tanga, kwa mfano, tunapotaka
kujenga Mahakama ni sehemu gani ambayo pengine idadi ya watu imeongezeka na sehemu
gani ambayo inazalisha mashauri mengi,”
amesema.
Jaji
Mkuu amebainisha kuwa jana akiwa katika ziara Wilaya ya Kilindi aliambiwa
changamoto ya kijiografia ya Wilaya hiyo kuwa haina sehemu ambayo ni katikati
ambapo kama ikijengwa Mahakama ya Wilaya sehemu yoyote ile bado itakuwa sehemu
mbali na sehemu zingine.
“Kwa
hiyo, huo ni mtihani ambao tumeuona. Vile vile tumeuona katika Wilaya ya Handeni.
Wilaya ya Handeni ipo karibu kabisa na njia ya kwenda Dar es Salaam na ukilinganisha
na makao makuu ya Wilaya bado ni mbali sana. Kwa hiyo sensa ya watu itatusaidia
sana katika kupanga upya mpango wetu wa ujenzi wa miundombinu,” amesema Mhe.
Prof. Juma.
Amemweleza
Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa hata zoezi linaloendelea la anuani za makazi ni muhimu
kwa sababu Mahakama ingependa kujua anayefungua shauri anaishi wapi, akitakiwa
kupelekewa kama wito ifahamike ni wapi na wananchi wanaotaka huduma ziwasilishwe
mlangoni kupitia posta itafahamika ni mlango namba ngapi na upo mtaa upi.
“Hivyo
zoezi hili ni muhimu sana na ndiyo maana nimewaomba viongozi wa Mahakama
kuhakikisha kwamba majengo yetu yanapata anuani. Hatuwezi kuwadai wanaofungua
mashauri waonyeshe anuani wakati sisi wenyewe hatuna anuani za makazi,” amesema.
Jaji
Mkuu ametaja kipaumbele kingine ambacho huiongoza Mahakama ni maeneo mapya ya
utawala. Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, kwa bahati mbaya Mahakama imekuwa
ikisahauliwa pale Serikali inapoanzisha mikoa na wilaya, wakati mwingine katika
maeneo hayo mapya rasilimali inatengwa kujenga vituo vya polisi, lakini mara nyingi
huduma za utoaji haki huwa zinasahaulika.
Amebainisha
kuwa ukiangalia katika Wilaya 20 ambazo Mahakama za Wilaya zimejengwa ni Wilaya
ambazo zilianzishwa bila rasilimali fedha kutengwa kwa ajili ya Mahakama mpya na
ndiyo maana zilichelewa kujengwa. Amesema hata zoezi zingine zinazofanywa na Serikali,
kwa mfano, kuhamisha watu kutoka Ngorongoro kwenda Wilaya ya Handeni, ni
changamoto ambayo itazaa mahitaji ya Mahakama.
“Tunaiomba
serikali mapema, mazoezi makubwa kama haya yanapofanyika Mahakama Mwanzo vilevile
zijengwe zenye hadhi kuwezesha hata Mahakimu wa Mahakama za Wilaya waweze
kutembelea maeneo hayo,” Jaji Mkuu amesema.
Amesema
kuwa shughuli za kiuchumi ni
kipaumbele kingine kinachotumiwa na Mahakama kujenga miundombinu ya majengo,
huku akibainisha kuwa zoezi la sensa litaonyesha wapi shughuli za kiuchumi
zimeongezeka. Aidha, Jaji Mkuu amesema mazingira ya kijiografia vile vile huangaliwa
ikizingatiwa kuna maeneo makubwa ambayo yanahitaji usafiri mgumu kufikia maeneo
ya utoaji haki.
Katika
siku ya tatu ya ziara yake, Jaji Mkuu ametembelea maeneo mbalimbali ya Lushoto
na Korogwe. Mbali na kukutana na Wakuu wa Wilaya hizo, Mhe. Prof. Juma ameongea
na watumishi wa Mahakama na kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa Mahakimu
Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya hizo.
Jaji
Mkuu anatarajia kuhitimisha ziara yake leo Tanga mjini. Mhe. Prof. Juma ameongozana na viongozi
mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Kevin Mhina, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama,
Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa
Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba.
Wengine
ni Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi
Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory
Kagaruki, mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes
Mombury, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Bw. Yohana Mashausi, Afisa Utumishi, Bw.
Jeofrey Mnemba, Mpima Ramani Abdallah Nalicho, Mhandisi Peter Mrosso na
Msaidizi wa Sheria wa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Hassan Chuka.
Kwa
upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa
Mansoor, Naibu Msajili Beda Nyaki, Mtendaji Humphrey Paya, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Sofia Masati, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Mhe. Ruth Mkusi na Msaidizi wa Sheria wa
Jaji Mfawidhi, Mhe. Grace Mwaikono.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto.
Viongozi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakifuatilia na kuchukua kumbukumbu za taarifa hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni