Na Magreth Kinabo- Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewaomba wananchi kujifunza masuala mbalimbali ya myororo wa utoaji haki kupitia vyombo vya habari ili kuweza kuwa uelewa wa elimu ya sheria kabla ya kufika mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake jijini Dar es Slaam, Prof. Gabriel alisema Mahakama ya Tanzania imeanza kutoa elimu ya sheria kila wiki katika kipindi cha SEMA NA MAHAKAMA YA TANZANIA kupitia vyombo vya habari, ambavyo ni Kituo cha Televisheni cha ( ITV) kila Jumanne kuanzia saa 12:30 jioni hadi 1:30 jioni,na Shirika la Taifa la Utangazaj (TBC1) kila Alamisi saa 12:00 jioni hadi saa 1:00 jioni, hivyo mada mbalimbali zitakuwa zikijadiliwa kupitia kipindi hicho.
Alisema tayari mada ya Mahakama ya Tanzania na Mpango wa Uboreshaji Huduma imeshatolewa na televisheni ya ITV kupitia kipindi hicho siku ya Jumanne ya Mei 17, mwaka huu na itarudiwa leo Alamisi Mei 19, mwaka huu kupitia Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC1).
“Tunawaomba wazazi, walezi walimu, wanafunzi na jamii kujifunza masuala haki kupitia kipindi hicho,” alisema Prof. Gabriel.
Aliongeza kwamba miongoni mwa mada itakayojadiliwa ni usimamizi wa mirathi na changamoto zake, ambapo elimu kuhusu mirathi, ndoa na talaka itatolewa, ikiwemo kuelea matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA) ili kupunguza makaratasi kwa kuwa hivi sasa kuanzia Septemba 19, mwaka huu Mahakama iliacha matumizi ya karatasi na kuanza kutumia ofisi mtandao.
Alifafanua kuwa tayari Mahakama ina mifumo ya pamoja inayofanana na ofisi ya Mwendesha Mashtaka nchini (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Polisi na Wizara ya Katiba na Sheria.
Aidha alisema kuwa wananchi pia wanaweza kupata kutoa maoni kupitia namba ya simu ya Kituo cha Kutoa Taarifa cha Huduma kwa Mteja (Call Center) ambayo ni 0752500400, na baruapepe maoni judiciary.go.tz. Prof. Elisante aliwaomba wananchi kutoa taarifa sahihi na uhakika ili Mahakama ifanyie kazi kwa kuwa imeanzisha huduma hizo ili kila Mtanzania apate haki kwa wakati.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Elisante Ole Gabriel akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake kuhusu uanzishaji wa kipindi cha SEMA NA MAHAKAMA YA TANZANIA, kitakachozungumzia masuala mbalimbali ya utoaji haki nchini kila wiki katika chombo cha habari cha televisheni ya TBC1 na ITV.
Picha na Magreth Kinabo- Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni