Alhamisi, 19 Mei 2022

KASI YA 4G YA MAHAKAMA USIKILIZAJI MASHAURI YAWASHANGAZA WANANCHI

· Mmoja Mahakama ya Rufani aandika ujumbe kulalamika

Na. Faustine Kapama, Mahakama, Tanga.

Wananchi wameanza kuilalamikia Mahakama ya Tanzania kwa kasi ya kutisha inayoendelea ya uondoshaji na usikilizaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali za Mahakama nchini kote.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 19 Mei, 2022 katika siku ya nne na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga.

Akizungumza na watumishi wa Kanda hiyo kwenye kikao cha majumuisho, Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa katika maeneo mengi Mahakama ya Tanzania imefanya vizuri hususani kwenye kuondosha mlundikano kiasi kwamba hata wenye mashauri wanalalamika kwa kasi iliyopo.

“Msajili wa Mahakama ya Rufani ameshalalamikiwa kwa sababu wale waliokuwa wamezoea kuleta rufani na kuzipaki wakijua baada ya miaka mitatu wataendelea na masisha yao kama kawaida wameanza kulalamika,” amesema.

Jaji Mkuu anaongeza, “Kuna mmoja alipopelekewa wito alilalamika kabisa na kunitumia ujumbe kwamba hapa lazima kuna masuala ya rushwa, huu mwendo sio wa kawaida, kwa nini mnatupangia tarehe ya kusikilizwa ndani ya wiki mbili. Kwa hiyo, hayo ni mafanikio makubwa sana, nawaomba tuendelee na kasi hiyo hiyo.”

Mhe. Prof. Juma ameishauri Kanda hiyo kwa upande wa Mahakama Kuu kuanzisha utaratibu wa kuchambua mashauri na kubainisha yale ambayo yanayoweza kusikilizwa bila ya gharama kubwa, yakiwepo mashauri yanayokuja kwa ajili ya kuchukua kiri au kataa (plea taking) na mashauri mengine yasiyo na mashahidi wengi.

“Kanda iendelee kuwatumia Mahakimu wenye Mamlaka ya Ziada (Extended jurisdiction) kusikiliza mashauri hayo. Nawaahidi kuwa uongozi wa Mahakama Makao Makuu utaendelea na jitihada za kupata fedha zaidi ili vikao vinavyopangwa kulingana na kalenda zenu visiathirike,” amesema.

Jaji Mkuu amesema kuwa katika ziara yake amebaini kuwa kasi ya usikilizaji wa mashauri ni nzuri, hivyo amewasihi watumishi wote kuendelea na kasi waliyonayo na kuhakikisha kuwa wanatimiza vigezo vya idadi ya mashauri vilivyopangwa.

Aidha, Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa maafisa wote wa Mahakama wanajukumu la kusimamia kwa madhubuti uendeshaji mashauri na kuzuia maahirisho ya mara kwa mara yasiyo na sababu za msingi.

“Msikubali kuahirisha mashauri kwa muda mrefu kwa ajili ya kuandaa maamuzi madogo yanayotokana na pingamizi ambazo nyingi zinatumiwa vibaya kwa lengo la ucheleweshaji. Msikubali kutumia taratibu za kimahakama pale mnapoona lengo la wahusika ni kuchelewesha shauri,” amesema.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu kutokuwa wepesi kukubali hoja za waendesha mashtaka kuwa upelelezi bado unaendelea bila kufafanua kitu gani katika upelelezi bado kinatafutwa na nani na kwa muda gani.

“Msiwe wepesi wa kukubali tu maelezo yanayotolewa kwamba upelelezi bado unaendelea, jalada lipo kwa RCO, unakubali tu, unampa mwezi, unampa wiki, hapana. Lazima aje na kiapo (aeleze) ni kitu gani bado kinatafutwa, ni nani mwenye huo ushahidi unaotafutwa. Haya maswali sioni mkiyauliza,”alisema.

Hivyo amesema umakini wa Mahakama ndio utahakikisha kuwa shughuli za upelelezi haziwanyimi wananchi haki ya kikatiba ya kutochelewesha haki yao ya kusikilizwa kesi bila sababu ya msingi.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, kwa kuwa Mahakama ni msimamizi wa haki ya kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu huru, ni wajibu wa Mahakama kutoa dhamana kwa makosa yenye dhamana.

“Vigezo vya kutumiwa kutoa dhamana ni pamoja na kutumia vitambulisho vya Taifa na vitambulisho vinavyokubalika na Mahakama ziwaruhusu washtakiwa kujidhamini wenyewe pale nmnapojiridhisha na utambulisho wao kuwa watahudhuria mahakamani. Anwani za makazi na vitambulisho vya uraia zisaidie kurahisha kutolewa kwa dhamana,” amesema.

Mhe. Prof. Juma ameshauri pia kuwa mashauri ambayo washtakiwa wamekosa dhamana yasikilizwe kwa haraka na kwamba sheria itumike ili kuyaondosha yale yenye makosa yasiyo na dhamana na yako ndani ya mamlaka ya Mahakama.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama, Kanda ya Tanga, Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa Mansoor amesema kuwa hadi kufikia mwezi Desemba 2021, Masjala ya Mahakama Kuu ilibaki na jumla ya mashauri 493 na kati ya Januari hadi Mei 12, 2022, jumla ya mashauri 246 yamefunguliwa, ambapo yaliyoamuliwa yalikuwa 433 na yaliyobaki yapo 306.

Amesema hadi kufikia Mei 12, 2022 Masjala ya Mahakama Kuu ilikuwa na jumla ya mashauri ya mlundikano 21 ambayo kati ya hayo, mashauri manne ni ya jinai na yote yamepangwa kusikilizwa kwenye kikao ambacho kimeanza tarehe 16 Mei, 2022. Mhe. Mansoor amemhakikishia Jaji Mkuu kuwa kufikia mwezi Julai hapatakuwepo na shauri hata moja la mlundikano kutokana na mkakati waliojiwekea wa kuondosha mashauri hayo.

Katika ziara yake, Jaji Mkuu ametembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya za Kilindi, Handeni, Lushoto, Korogwe, Mkinga na Tanga mjini.  Katika maeneo yote, Mhe. Prof. Juma alipata nafasi ya kukutana na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Adam Malima, Wakuu wa Wilaya zote, kukagua ujenzi wa Mahakama mbili za Wilaya ya Kilindi na Mkinga, kupokea taarifa za kiutendaji  na kuzungumza na watumishi.

Jaji Mkuu aliongozana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba.

Wengine ni Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory Kagaruki, mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Bw. Yohana Mashausi, Afisa Utumishi, Bw. Jeofrey Mnemba, Mpima Ramani Abdallah Nalicho, Mhandisi Peter Mrosso na Msaidizi wa Sheria wa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Hassan Chuka.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa Mansoor, Naibu Msajili Beda Nyaki, Mtendaji Humphrey Paya, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Sofia Masati, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Mhe. Ruth Mkusi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Grace Mwaikono.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongea na watumishi leo tarehe 19 Mei, 2022 katika siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor akisistiza jambo.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina akitoa utambulisho wa viongozi wakuu katika mkutano huo.

Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizoibuliwa na watumishi.

Mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury akiwasilisha taarifa yake kwenye mkutano huo.

Viongozi waandamizi wa Mahakama wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na watumishi katika mkutano huo. Kutoka kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory Kagaruki, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury.
Sehemu ya watumishi (picha ya juu na chini) ikifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo kwenye picha).


Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa kada mbalimbali (juu) na Mahakimu Wakazi (chini)   baada ya mkutano huo.










Hakuna maoni:

Chapisha Maoni