Alhamisi, 19 Mei 2022

JAJI MKUU AHITIMISHA ZIARA YAKE KANDA YA TANGA

·       Aipongeza  Kanda kwa kutokuwa na mlundikano wa mashauri

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo terehe 19 Mei, 2022 amehitimisha ziara yake ya kikazi Mahakama Kanda ya Tanga huku akiwapongeza Watumishi wa Kanda hiyo kwa mafanikio mbalimbali ikiwemo ya kuondoa mlundikano wa Mashauri pamoja na kuzingatia Maadili na nidhamu.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama wa Kanda hiyo katika kikao cha Majumuisho ya ziara yake ya siku nne (4), Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, baada ya kukamilisha ziara yake ameridhishwa na masuala 11 kuhusu Kanda hiyo.

Baada ya siku nne za ziara yangu hapa Kanda ya Tanga nimeridhishwa na kazi zilizofanyika haswa katika maeneo ya kuondoa milundikano, milundikano iliyopo ni mashauri yaliyo nje ya uwezo wa Mahakama za Mahakimu, kutokuwa na mlundikano kutokana na kuongezeka kwa kasi ya uondoaji wa mashauri ukilinganisha na hapo nyuma,” amesema Jaji Mkuu.

 Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa, katika taarifa zote za Mahakama za Wilaya nane (8) za Mkoa wa Tanga amebaini kuwa hakuna mlundikano na hali ya uondoshaji wa mashauri iko vizuri, huku akiongeza kuwa hata baada ya kuwatembelea Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo wote wamekiri kuwa Mahakama inatekeleza majukumu yake ipasavyo na kwamba Watumishi wanazingatia pia maadili katika utendaji kazi wao kwakuwa hakuna masuala ya kinidhamu yaliyofikishwa
kwenye kamati zao
yanayowahusu watumishi wa Mahakama.

 Mhe. Jaji Mkuu amebainisha maeneo mengine aliyoridhishwa nayo katika Kanda hiyo ni kupunguza idadi ya Mahabusu gerezani, Mahakimu kufanikiwa kuchapa hukumu wenyewe na hivyo kupunguza mlundikano wa kazi za uchapaji kwa Katibu Muhtasi baada ya kupatiwa kompyuta mpakato ‘laptops na Mwajiri;

Mengine ni Kusajili mashauri kimtandao, kuhuisha taarifa katika Mfumo wa Uendeshaji Mashauri Kimtandao (JSDS 2) kwa wakati; kusajili na kuhuisha mashauri ya Mahakama za Mwanzo katika mfumo uitwao ‘Primary Court App’ kwa asilimia zaidi ya 85.

 “Matumizi ya TEHAMA kwa Kanda hii ni mazuri napenda kuipongeza Idara husika, kwa kuwa, kila tulipopita tumehakikishiwa na Naibu Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Essaba kuwa mko vizuri na taarifa zenu  zinauhishwa kwa wakati,” amepongeza Jaji Mkuu.

Vilevile, Mhe. Prof. Juma ameeleza kuridhishwa na hali nzuri ya Nidhamu; kuendeleza kwa utaratibu wa kutoa elimu kwa umma mara moja au mbili kila wiki; Kuimarisha hali ya mahusiano na wadau wa Mahakama; maendeleo mazuri ya miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama Kilindi na Mkinga.

Akiwasilisha taarifa ya Kanda, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor amemshukuru Jaji Mkuu kwa kutenga muda na kuamua kufanya ziara ambapo amekiri kuwa ziara hiyo imeleta suluhisho kwa baadhi ya changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo.

“Mhe. Jaji Mkuu tunashukuru kwa ujio wako katika Kanda hii ambao umeleta majibu ya changamoto tulizo nazo, pamoja na mafanikio tuliyonayo Kanda ya Tanga, bado kuna baadhi ya changamoto tunakabiliana nazo ambapo ni pamoja na upungufu wa Watumishi, ukosefu wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Tanga na megineyo ambayo tunaamini yatapatiwa ufumbuzi,” amesema Mhe. Mansoor.

 Katika siku ya mwisho ya ziara hiyo ililolenga kukagua maendeleo ya jukumu la utoaji haki ndani ya Kanda ya Tanga, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma alitembelea Ofisi ya Wilaya ya Mkinga na vilevile alipata nafasi ya kukagua Mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Mkinga.

 Mhe. Prof. Juma alitembelea pia wilaya zote nane za mkoani Tanga ambapo alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa maneneo hayo na kupokea changamoto zinazowakabili na kuwaahidi watumishi hao kuwa Changamoto zilizowasilisha zimechukuliwa na zitafanyiwa kazi inavyostahili.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis  Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Mahakimu wa Mahakama mbalimbali Kanda ya Tanga. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Dkt. Ubena, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi na wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T),  Mhe. Kevin Mhina. Zoezi la upigaji picha lilifanyika leo tarehe 19 Mei, 2022 baada ya kikao cha majumuisho ya ziara ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis  Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkinga
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Kushoto akiwasalimia Watumishi wa Mahakama Kanda ya Tanga wakati alipowasilia katika Mahakama hiyo kwa ajili ya kikao cha Majumuisho na watumishi hao.

Katika siku ya mwisho ya ziara yake, Jaji Mkuu, Prof. Juma alipata fursa ya kukagua Mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Mkinga-Tanga (katika picha).
Ukaguzi wa jengo ukiendelea, kulia ni Mkuu wa Kitengo cha usimamizi wa Majengo-Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Yohana Mashausi. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis  Juma (katikati) akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Tanga (hawapo katika picha).

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Tanga wakimsikiliza Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma (hayupo katika picha).
Sehemu ya Maafisa walioambatana na Jaji Mkuu wakimsikiliza alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara.
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi akijibu hoja za watumishi wa Mahakama Kanda ya Tanga wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Tanga wakiwa katika kikao hicho.



 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni