Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ngerengere
iliyopo Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mbaraka Mchopa hivi karibuni aliongoza kikundi
cha wanamazingira kwa kushirikiana na watumishi kupanda miti katika eneo la
wazi la Mahakama hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhe. Mchopa
alisema kuwa walipata msukumo wa kupanda miti baaada ya kuona zoezi la namna hiyo
lililoendeshwa kwa mafanikio makubwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe.
Alisema kuwa Mhe. Ngwembe aliendesha zoezi kama hilo
la upandaji miti katika eneo la wazi kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani
hapa hivi karibuni.
“Baada ya zoezi
lile niliomba miti kupitia kikundi cha mazingira cha Mgambo ambapo walitupatia
miti 107 bure ili kuunga juhudi hizi za utunzaji wa mazingira na kuhifadhi
maeneo ya wazi ya Mahakama kwa matumizi ya baadae” alieleza.
Aidha, Mhe. Mchopa alisema kuwa kikundi cha mazingira
cha Mgambo hakikuishia kutoa miti pekee bali kilishiriki kikamilifu kwenye
zoezi la upandaji na kutoa ushauri wa
namna bora ya kuhifadhi miti hiyo ili iweze kukua.
Miti iliyopandwa ni jamii ya Misedelea, Mikongo na
Mikaratusi, ambayo kwa mujibu wa Mhe. Mchopa, itahudumiwa na washtakiwa
wanaopewa adhabu mbadala za kutumikia jamii chini ya usimamizi wa Mahakama
hiyo.
Akitoa maoni yake kuhusu hatua hiyo, Mhe. Ngwembe amelipongeza
zoezi lililofanywa na Mahakama hiyo na kutoa agizo kwa Mahakama zote zilizopo
katika Kanda yake kuhakikisha zinapanda miti katika maeneo yote ya wazi ili
kuyahifadhi.
Jaji Mfawidhi huyo amesisitiza kuwa miti yote
itakayopandwa iwe ni miti ya faida kama matunda au itakayotumika kwa mbao siku
za usoni.
“Nilielekeza na ninaelekeza tena kila Hakimu aliyepo
kwenye Kanda hii ahakikishe anapanda miti kwenye maeneo ya wazi ya Mahakama, sio
kupanda miti tu bali kuhakikisha wanaitunza miti hiyo,” alisema
Jaji Mfawidhi huyo aliongeza, “Kama umepanda miti
100 leo hakikisha unatukabidhi miti 100 ikiwa hai baada ya miezi 9, miti
itakayokufa itolewe na kupandwa mingine.”
Ikumbukwe tarehe 6 Mei, 2022, Mhe. Ngwembe aliongoza
zoezi la kupanda miti eneo la wazi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani
hapo kama kampeni ya kutunza maeneo yote ya Mahakama kwa ajili ya matumizi ya
kizazi cha kijacho. Zoezi hilo
lilipokelewa vyema na sasa jitihada za kuungwa mkono zinafanyika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni