Na Ahmed Mbilinyi-Mahakama, Bukoba
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga amewataka watumishi wa Kanda hiyo
kuungana kwa pamoja na kusaidiana kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya
Tanzania wa mwaka (2020/2021 – 2024/2025) ili mhimili huo uweze kufikia malengo
yake kwa ufanisi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la
Wafanyakazi wa Kanda hiyo kilichofanyika hivi karibuni, Mhe. Kilekamajenga
alisema kuwa ili kufikia malengo na kufanikisha utekelezaji wa mpango huo ni
muhimu kushirikiana na kufanya shughuli zote za kimahakama kwa upendo.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya
Bukoba, Bw. Lothan Simkoko aliwaambia watumishi kuwa mpango mkakati huo utashushwa
kwa kila ngazi ya Mahakama ili waweze kufanya kazi katika njia moja na hatimaye
kuifikia azma ya Mahakama ya kutoa haki kwa wakati.
Ulitolewa msisitizo katika kikao hicho
kilichowashirikisha watumishi wote wa Mahakama katika kila ngazi kuhusu umuhimu
wa kila mtumishi kuujua mpango mkakati wa Mahakama 2020/21 – 2024/25 ili kurahisisha
utekelezaji wake.
Katika mkutano wa Baraza hilo, wajumbe
waliafikia jumla ya maazimio saba (7) yachukuliwe na wapelekwe kwenye kikao cha
Baraza la Wafanyakazi Taifa, ikiwemo watumishi wote wa Mahakama kuwekwa kwenye
mfumo mmoja wa malipo ya mshahara yaani “TJS”.
Pia waliazimia watumishi wote wapatiwe stahili
za malipo ya ‘court attire’ na sio malipo hayo kutolewa kwa Mahakimu pekee,
watumishi kupatiwa posho mbalimbali zitakazokuwa zinaingizwa moja kwa moja
kwenye akaunti zao, mfano posho ya chakula, posho ya mazingira magumu ili
kuweza kuwasaidia watumishi kutokana na kuwa na viwango vidogo vya mshahara.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Bukoba, (katikati) ,Mhe Dkt Ntemi Kilekamajenga akifungua kikao cha
Baraza la wafanyakazi Kanda ya Bukoba.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw.
Lothan Simkoko akiwasilisha mada ya mpango mkakati wa Mahakama 2020/21 –
2024/25
Katibu wa Tughe Mkoa wa Kagera, Bw. Edward
Mwashitanda akichangia mada katika Baraza la wafanyakazi Kanda ya Bukoba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni