Jumatatu, 9 Mei 2022

WATUMISHI WANAWAKE MAHAKAMA SHINYANGA WATOA MSAADA KWENYE KITUO CHA KULELEA WAZEE KOLANDOTO

Na Emmanuel Oguda – Shinyanga

Watumishi wanawake wa Mahakama, Kanda ya Shinyanga wakiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elizabeth Mkwizu hivi karibuni walitembelea kituo cha kulelea wazee wasiojiweza kilichopo Kata ya Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga na kutoa msaada wa vitu mbalimbali.

Akizungumza na wazee hao, Mhe Mkwizu alisema kuwa watumishi hao wa Mahakama waliguswa na mahitaji katika kituo hicho na kuamua kuhamasishana kutoa michango na kufanikiwa kununua baadhi ya vitu kwa ajili ya kuwasaidia katika mahitaji yao.

“Kuelekea siku ya akina mama, sisi wanawake watumishi wa Mahakama Shinyanga tuliguswa kushiriki kuwafariji wazee wetu mnaoishi katika kituo hiki, tulihamasishana na kufanikiwa kununua baadhi ya vitu kwa ajili ya mahitaji katika kituo hiki. Tutavikabidhi kwenu ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wanaoshiriki katika kuwatunza,” alisema.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavisi Miti alisema kuwa kituo hicho kina mahitaji mengi lakini kupitia michango yao watumishi hao waliweza kununua friji moja itakayosaidia kuhifadhi vyakula mbalimbali, mashine ya kufulia na kukausha nguo, mchele, viazi, sabuni na mifagio, vyote vikiwa na  thamani ya zaidi ya milioni mbili.

Akiongea kwa niaba ya wazee hao, Mzee Shadrak Mhoja aliwashukuru watumishi hao wa Mahakama kwa kutambua mahitaji ya kituo hicho na kuwapelekea vitu vikubwa ambavyo wao hawakutegemea kuvipokea. “Tunashukuru sana, kwetu sisi hivi ni vitu vikubwa, Mungu awabariki na sisi tumefurahi,”alisema Mzee Mhoja.

Akitoa salamu za Shukrani, Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga, Bi. Elizabeth Mweyo aliwapongeza wanawake wa Mahakama kwa kutoa msaada huo kwa jamii kwa vile vifaa vilivyotolewa vitasaidia kukidhi baadhi ya mahitaji ya wazee hao.

 “Tunashukuru sana kwa msaada huu, tunawaomba wadau wengine mbalimbali waendelee kukisaidia kituo hiki kwani bado kunauhitaji katika maeneo kadhaa, ikiwemo ukarabati wa baadhi ya mabweni ya wazee pamoja na ujenzi wa bweni moja ili liweze kukidhi hali halisi ya wazee wetu katika kituo hiki,” alisema.

Awali akitoa taarifa fupi, Afisa Mfawidhi wa Kituo Bi. Sophia Kang’ombe, ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii Shinyanga alieleza kuwa kwa sasa kituo hicho kina wazee 15 wasiojiweza na wenye mahitaji maalum ambao wamekuwa wakilelewa hapo kwa mchango wa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Makundi Maalum na wadau mbalimbali.

Alisema kuwa wadau hao wamekuwa wakitoa misaada ya vitu mbalimbali ikiwemo vyakula na nguo na ukarabati wa majengo pamoja na matibabu kwa wazee hao ambao kwa sasa wote wana bima ya matibabu CHF na wanapatiwa matibabu katika hospitali teule ya Kolandoto katika Manispaa ya Shinyanga.

Kituo cha kulelea wazee wasiojiweza na wenye uhitaji maalum Kolandoto Shinyanga kilianzishwa mwaka 1975. Kituo hicho kipo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga ambacho hutoa huduma kwa wazee wasiojiweza, wasio na ndugu na wenye mahitaji maalum.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Elizabeth Mkwizu (aliyesimama) akiongea na wazee wakati watumishi wanawake wa Mahakama Shinyanga walipowatembea katika makazi yao. Kutoka kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe. Mary Mrio, Afisa Mfawidhi wa Kituo Bi. Sophia Kang’ombe, Mtendaji wa Mahakama Kuu Bi. Mavis Miti na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ibadakuli, Mhe. Irene Makundi.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti akieleza dhumuni la wanawake watumishi wa Mahakama Shinyanga kutembelea kituo hicho.

Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Kolandoto Shinyanga, Bi. Sophia Kang’ombe akitoa taarifa fupi baada ya kutembelewa na watumishi wanawake wa Mahakama Shinyanga.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Elizabeth Mkwizu akikabidhi zawadi kwa akina mama wazee waliopo katika kituo hicho.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Elizabeth Mkwizu akikabidhi jokofu pamoja na mashine ya kufulia na kukausha nguo kwa wazee katika kituo cha Kolandoto kwa niaba ya watumishi wanawake wa Mahakama Shinyanga.

Mzee Zengo akisakata rumba kwa furaha na baadhi ya watumishi wanawake wa Mahakama  baada ya kupokea vitu hivyo.

Baadhi ya wazee waliopo katika kituo cha Kolandoto Manispaa ya Shinyanga.

Watumishi wanawake wa Mahakama Shinyanga katika picha ya pamoja na wazee waliopo katika Kituo cha kulelea wazee Kolandoto Manispaa ya Shinyanga.

Baadhi ya Watumishi wanawake wa Mahakama Shinyanga walioshiriki zoezi la kukabidhi vifaa na mahitaji mbalimbali kwa wazee katika kituo hicho.

Watumishi wanawake wa Mahakama Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni