Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. George Masaju amewaasa
Wahasibu na Wakanguzi wa Ndani kutumia mafunzo waliyapata yawe chachu ya
mabadiliko kiutendaji kwa kutenda haki kwa wote bila kujali hali zao za
kiuchumi na kijamii, ukilenga kuongeza na kuimarisha utekelezaji wa Mpango
Mkakati wa Mahakama 2020/2021 hadi 2024/2025 kwa kasi zaidi.
Akifunga
mafunzo hayo ya kundi la pili lilokuwa na washiriki 55 yaliyoendeshwa kwa muda
wa siku tano katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji jijini Dodoma leo
tarehe 10 Juni 2022, Jaji Masaju alisema, maneno haya ya kikatiba ya kutochelewasha
haki bila sababu ya kimsingi ndiyo yanaunda dira ya Mahakama ya Tanzania
inayosema upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa wote.
“Wahasibu
na Wakaguzi wa Ndani mnahusika sana katika mchakato wa utoaji haki kwa wakati,
kila mmoja wenu kwa hatua yake akichelewesha mchakato wa matumizi ya fedha dira
hii haitafanikisha adhima yake, msidhani anayeweza kuchelewa haki ni Jaji,
Msajili, Hakimu au Mtengaji hata ninyi ni sehemu muhimu sana kiutendaji”,aliongeza
Mhe. Masaju
Jaji
Masaju akaendelea kusema, katika Muhimili huu watu wote tunategemeana na kila
mtu ana nafasi yake ili kutekeleza dira awe Mlinzi, Dereva, Muhudumu, Karani na
kada zote, mathalani bila mlinzi kuwepo ofisi ikaungua au mafaili yote
yakaibiwa maana yake huduma hazitatolewa.
“Msiende
kufanya kazi zenu kwa mazoea ya awali mbadilike na mkawe chachu ili kwenda
sambamba na maboresho yanayoendelea ndipo mtaweza kuutekeleza Mpango Mkakati wa
Mahakama wa 2020/2021 – 2024/2025 kwa kuwa tayari mna uelewa mpana wa majukumu
yanayopaswa kutekelezwa kwa kasi zaidi. Hivyo basi, Wahasibu na Wakaguzi wa
Ndani kile kitu mnachoweza kukifanya kwa ufanisi na kwa wakati ili kusaidia
upatikanaji wa haki kwa mwananchi tukifanye kwa weledi na kwa wakati ipasavyo”,
alibainisha Mhe. Jaji
Katika
Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania kama ilivyofanyiwa
marekebisho mara kwa mara, inaongelea usawa mbele ya sheria watu wote ni sawa mbele
ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa
mbele ya sheria ni wajibu wenu Wahasibu kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi
wa aina yoyote bila kujali hali zao na hapo ndipo mtakuwa mnatekeleza dira ya
Mahakama, alinukuu Jaji Masaju.
Mhe.
Masaju akazungumzia changamoto daima ni sehemu ya maisha, katumieni elimu
mliyoipata kutatua changamoto za kimtandao badala ya kuwa walalamikaji. Mfano,
unaposhindwa kukusanya maduhuli kwa njia ya POS jiulize utakuwa umepoteza kiasi
gani cha fedha za serikali. Kuweni na tabia ya kubadilishana mawazo na vituo
vingine badala ya kukaa na tatizo lako.
“Daima
wasilianeni, shaurianeni Kanda na Kanda, Mkoa na Mkoa. Wasaidieni viongozi wenu
kutekeleza majukumu yao katika kupanga na kutumia fedha za ofisi zenu. Nyie ndiyo
washauri wakuu wa maafisa Masuhuli “Sub-warrant Holders” katika mambo ya fedha,
hivyo tunawategemea. Toeni ushauri wa kitaalam na sio kwa woga”, alitoa rai
Jaji Masaju.
Aidha,
Jaji Masaju alisema, Dunia ya sasa ipo katika wimbi la nne la maendeleo ya
viwanda inayohusisha matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA).
Mfahamu kuwa hata mifumo ya utendaji kazi mliyoisoma kupitia mafunzo
yaliyomalizika imejikita katika matumizi ya TEHAMA.
“Hivyo,
niungane na viongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania kuwataka kuendelea
kujifunza mifumo yote inayotengenezwa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu
yetu. TEHAMA si tu inarahisisha utekelezaji wa majukumu bali inasaidia katika
kuwafikia wananchi kwa wingi na kwa muda mfupi kwa mfano katika ukusanyaji wa
maduhuli tunatumia Mashine za POS zenye mifumo ya TEHAMA. Ninawaasa zinapotokea
changamto za mifumo hiyo jitihada za utatuzi zifanyike haraka ili kuepuka
kuchelewesha huduma na kupoteza mapato ya serikali”, alisisitiza Mhe. Masaju.
Mafunzo
hayo ya awamu ya pili kwa kundi la Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani inatokana na
moja ya utekelezaji malengo kimkakati ya Mahakama ya Tanzania iliyoweka wa
kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama wa ngazi zote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni