Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 8 Juni 2022 aliendelea kufanya usaili kwa kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa wanafunzi 321 waliofaulu mitihani yao katika Shule ya Sheria kwa vitendo na Baraza la Elimu ya Sheria wanaoomba kuorodheshwa kwenye daftari la Mawakili.
Waombaji hao kutoka Kanda
za Dodoma na Tabora walifika mbele ya Jaji Mkuu kwa njia ya mtandao kupitia
miundombinu iliyowekwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora na Kituo
Jumuishi cha utoaji haki Dodoma na kufanya usahili, hivyo kuokoa muda,
gharama na usumbufu wa kusafiri kwenda
jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Arnold Kirekiano, takribani waombaji 152 kutoka
Dar es Salaam, Mtwara, Tanga Dodoma na Tabora tayari wamekwishafika mbele ya
Jaji Mkuu kufanyiwa usahili huo. Zoezi hilo linaendealea katika vituo
vingine vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda za Mwanza, Bukoba, Arusha na Mbeya
ambapo waombaji wengine takribani 160 kutoka maeneo ya jirani watafanyiwa
usahili huo unaoendelea nchi zima kulingana na Kada hizo.
Mhe. Kirekiano amesema kwa sasa zoezi limeenda vizuri kwa
kuzingatia kwamba nchi yetu ni kubwa uwepo wa vifaa vya TEHAMA katika kila
kituo cha Mahakama Kuu Kanda husika vimesaidia kufanikisha zoezi hilo. Aidha,
alimshukuru Jaji Mkuu kwa kuruhusu zoezi hilo kufanyika kwa njia ya TEHAMA.
Naye mmoja wa washiriki wa usahili huo, Wakili mtarajiwa Bi. Mwanabibi Kalambo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa juhudi zake za kuhimiza na kukuza matumiza ya TEHAMA katika kutekeleza majukumu yake.
“Nadhani ni jambo zuri sana kwa Mahakama kukuza matumizi haya ya mfumo wa
mawasiliano, nawaza kama nigesafiri kutoka Dodoma hadi Dar es salaam
ningetumia gharama kubwa na muda ungekuwa mrefu na washiriki kwa vile tungekuwa wengi
sehemu moja. Matumizi ya TEHAMA
yamesaidia kuokoa muda, gharama na kuondoa usumbufu kwani mahojiano
yalichukua muda mfupi sana na mawasiliano yalikuwa ya kiwango bora”, alisema
Mwanabibi
Sherehe ya kuwapokea na kuwakubali Mawakili hao wapya, kula
kiapo cha uadilifu na kuorodheshwa
kwenye daftari la Mawakili inatarajiwa kufanyika tarehe 8 Julai, 2022 jijini Dar
es Salaam, huku mgeni rasmi akiwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni