Na Faustine Kapama – Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 8 Juni, 2022 ametembelea Gereza
la Ukonga na kukutana na viongozi wa Magereza kwa lengo la kujifunza mambo
mbalimbali na kuimarisha ushirikiano uliopo ili kuboresha mnyororo wa utoaji
haki wa wananchi.
Prof. Ole Gabriel aliwasili katika
maeneo ya Gereza hilo majira ya saa 3.00 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji
wake, Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Josephat Mkama ambaye
aliambatana na Mkuu wa Gereza la Keko, Kamishna Msaidizi wa Magereza Rashid Mtimbe
na Mkuu wa Gereza la Segerea, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hamis Lissu.
Baada ya kusalimiana na viongozi
hao, Mtendaji Mkuu wa Mahakama alielekea ofisini kwa Mkuu wa Gereza na kupata
taarifa fupi na baadaye kuzungukia maeneo kadhaa ya Gereza hilo ambapo
amejionea mambo mengi na kazi nzuri za mikono zinazofanywa na wafungwa wanaotumikia
vifungo mbalimbali.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Prof.
Ole Gabriel ameupongeza uongozi mzima wa Magereza kwa mapokezi mazuri
waliyompatia yeye pamoja na maafisa alioongozana nao na kwa fursa hiyo kwa
ujumla ambapo ameahidi kuwa Mahakama ya Tanzania itafanya kila linalowezekana kutoa
mchango wake ili kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
“Tumejifunza mengi, hii ni fursa
nzuri ya kuona jinsi gani tunaweza kushirikiana kwa kutambua kwamba ule
mnyororo wa haki una wadau wengi, wakiwemo Magereza, Polisi, Waendesha
mashtaka, Mahakama na wengine. Tumeanzisha utaratibu wa kuwa na mazungumzo ya
pamoja ili kubaini maeneo ambayo tunaweza kushirikiana ili Mtanzania apate haki
yake kwa haraka na kwa wakati,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema
kuwa jambo jingine ambalo amejifunza ni jinsi Magereza, ukiachilia mbali shughuli
za utoaji haki kwa wananchi, inajishughulisha pia na uzalishaji wa vitu vingi vizuri,
ikiwemo Samani ambazo ameziona na kurithika kuwa zinafaa kwa matumizi
mbalimbali.
“Nisema tu kwamba sitasita hata
kidogo kutumia samani zinazotengenezwa na Magereza yetu kwenye baadhi ya
majengo yetu ya Mahakama mpya tunazojenga ambazo ni nyingi, hivyo hii ni moja
ya fursa,” alisema.
Kuhusu kuboresha mnyororo wa haki,
Prof. Ole Gabriel amewaambia viongozi hao wa Magereza kuwa Mahakama imeanzisha kituo
maalumu cha Call Centre tangu Machi mosi mwaka huu kwa lengo la kupata mrejesho
kutoka kwa wananchi wa huduma zinazotolewa katika maeneo mbalimbali ya
kimahakama.
“Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim
Hamis Juma amekuwa akisisitiza suala la uwazi katika myororo wa haki na kupata
mrejesho. Hata Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan amesisitiza suala la kuendelea kufuatilia ili mwenye haki na
apate haki yake. Hivyo tumeamua kuanzisha call centre ambayo inafanya vizuri,”
amesema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
akabainisha kuwa kufuatia hatua hiyo Mahakama itaandaa utaratibu salama
utakaowawezesha Wafungwa na Mahabusu waliopo katika magereza mbalimbali kutoa
mrejesho wao kadri wanavyoona kutokana na huduma zinazotolewa na ngazi
mbalimbali za Mahakama.
“Wazo hili limepokelewa vizuri na
wenzetu wa Magereza, tumeweka mfumo mzuri ambao utakaowawezesha hata wananchi
walipo katika Magereza waweze kutupa mrejesho ili tuone kuna nini ambacho
tunaweza kuendelea kukiboresha,” alisema.
Hata hivyo, Prof. Ole Gabriel
aliwakumbusha wananchi kuwa utaratibu huo ulioanzishwa sio mfumo mwingine wa
kukata rufaa uamuzi uliotolewa na Mahakama, bali ni kutoa haki ya kuendelea
kutoa mrejesho wa huduma zinazotolewa na Mahakama katika ngazi yoyote kuanzia
Mahakama ya Mwanzo.
Hivyo amewasihi wananchi kokote
walipo kuchangamkia fursa hiyo kwa kutumia njia rahisi za mawasiliano ikiwemo
simu ya kiganjani namba 0752500400 na barua pepe ambayo ni maoni@judiciary.go.tz, huduma ambazo zinatolewa
masa 24 na siku saba kwa kila wiki.
Baada ya kufanya ziara hiyo,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama alielekea katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni
kuzungumza na watumishi wa Mahakama wanaofanyakazi katika Call Centre hiyo. Hakimu
Mkazi Mfawishi wa Kituo hicho, Mhe. Franco Kiswaga ameahidi kushirikiana na
watumishi wote ili Call Centre hiyo iweze kukidhi matarajio yaliyokusudiwa.
Katika ziara yake, Prof. Ole Gabriel
aliambatana na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Victoria
Nongwa, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili,
Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi Beatrice
Patrick, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu
Essaba na viongozi wawili kutoka Call Centre, Mhe. Domician Mlashani na Bi. Evetha
Mboya.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na askali Magereza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni