Na Magreth Kinabo - Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam Mhe.Jaji Amir Mruma amewataka watumishi
na viongozi wa Kituo cha Utoaji wa Haki (IJC) Kinondoni kuendelea kutoa huduma
bora za haki na zilizotukuka kwa wananchi ili kuweza kukidhi matarajio na
kujenga imani yao juu Mahakama.
Akizungumza jana tarehe 6
Juni, 2022 wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya Huduma kwa Mteja ya awamu
ya pili yanayowashirikisha watumishi na viongozi wa IJC hiyo ambayo
yanafanyika katika Kituo hicho jijini Dar es Salaam, Jaji Mruma alisema
upatikanaji wa haki ni imani kwa wananchi.
“Niwaombe watumishi wote
kuzingatia mafunzo na maelekezo yote yatakayotolewa na tuyatafsiri kwa kila
moja wetu kwa kutoa huduma kwa weledi na kwa kiwango cha hali juu ili huduma
zetu ziendane na ubora wa jengo lenyewe. Hivyo kila mtu anaowajibu wa
kuhakikisha haki inatendeka,” alisema na kuwasihi waendesha mashtaka na
mawakili nao kuisaidia Mahakama ili iweze kutekeleza jumkumu lake kikamilifu.
Aliwaambia watumishi hao kuwa ikiwa
kila mmoja atatimiza wajibu wake katika kutoa huduma atakuwa amejiinua yeye
mwenyewe, atainua kituo cha IJC na huduma za Mahakama za Tanzania kwa ujumla.
“Uboreshaji wa Mahakama unamlenga
mwananchi ambaye ni mteja wetu na namna Mahakama inavyomhudumia. Kwa hiyo,
kipaumbele cha Mahakama kinakuwa ni kutoa huduma bora zitakazofanya wananchi
kuwa na imani na chombo hiki cha haki pamoja na kuwaweka karibu na Mahakama. Kwa
dhamira hii, Mahakama inatutaka kubadili fikira zetu ili kuondokana na kutoa
huduma kwa mazoea.
“Badala yake kupitia mafunzo haya
tunakumbushwa kuwa kila mmoja wetu katika nafasi yake kuhakikisha anaunga mkono juhudi hizi za Mahakama kwa kutoa
huduma bora zitakazoendana na ubora na ukisasa wa jengo na mazingira yote
tunayofanyia kazi zetu.’’ alisisitiza.
Alifafanua kuwa
huduma bora zitakwenda sambamba na matumizi ya teknolojia ya kisasa ambayo
Mahakama imeipa kipaumbele cha hali ya juu. Mahakama ina mifumo ya Teknolojia
ya Habari na Mwasiliano(TEHAMA) ambapo matumizi yake katika kutoa huduma za kimahakama
imeshika kasi.
“Hivyo Kinondoni
tutaendelea na juhudi hizi ambazo tayari tunazitumia na kamwe hatutarudi nyuma.
Nawahimiza watumishi wote kuhakikisha mnajitoa katika kutumia TEHAMA ili wote
tuweze kuendana na kasi na tusiache mtu nyuma,’’ alisema.
Alisema teknolojia hiyo inawezesha kuchukua
ushahidi popote pale mtu alipo na kupunguza gharama za mteja na kwa Mahakama
kupunguza gharama za uendeshaji.
Jaji Mruma alisema kwamba, mafunzo
hayo ni nafasi ya kipekee iliyowakutanisha kupata uelewa wa pamoja katika azma
ya kuboresha zaidi utendaji wa kazi, hivyo ni nafasi adimu ambayo itawafanya
washiriki wote wa mafunzo hayo kutoa huduma zilizo bora na kwa kiwango cha juu
zaidi ili kumfanya mwananchi aweze kufurahia sio tu majengo na miundo mbinu
mizuri bali pia kupata huduma bora na kwa wakati.
Alizitaja faida za mafunzo hayo
kuwa ni kuboresha utendaji wa kazi, kupata maarifa mapya, kujenga mahusiano
mazuri na makundi tofauti na kupata marafiki wapya na kubadilisha mtazamo wa
utendaji kazi.
Mafunzo hayo ni njia ya kuondoa
changamoto na kukupa mwelekeo katika kuendeleza juhudi kwa yale yaliyofanikiwa
zaidi au kwa kutafuta njia mbadala za kutatua changamoto zilizojitokeza. Hivyo
ni matarajio yake kuwa mafunzo hayo yataboresha uwezo wa watumishi wote.
Wakati huohuo,
Mary Gwera anaripoti
kutoka Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Temeke kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Ilvin Mugeta amefungua mafunzo ya namna hiyo ambayo yamelenga kuwafahamisha
watumishi maana ya vituo hivyo na kuwaandaa kifikra na kisaikolojia ili wawe na
utayari wa kutoa huduma kama iliyokusudiwa.
Jaji Mugeta ambaye ndiye Mfawidhi
wa Kituo hicho alisema kwamba uboreshaji wa utoaji huduma katika nyanja zote yanatokana na mipango ya
mikakati madhubuti, uongozi imara pamoja na utayari na uthubutu wa watumishi
wote.
Aliongeza kuwa kwa kuwa wapo tayari wanaweza kuthubutu, hivyo amewahimiza kubadilika kwa kutekeleza majukumu yao kiuadilifu,weledi na kuwajibika ili wananchi waweze kuwaamini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni