Na Faustine Kapama– Mahakama, Mtwara
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewahimiza wadau mbalimbali katika mnyororo wa
utoaji haki nchini, hususani vyombo vya upelelezi kuzingatia sheria, miongozo
na taratibu zilizowekwa ili kuwezesha mchakato wa upelelezi na usikilizaji wa mashauri
kwenda kwa wakati, hivyo kuepuka kuchelesha utoaji wa haki kwa wananchi.
Mhe. Siyani ametoa rai hiyo leo tarehe
20 Juni 2022 katika siku ya kwanza ya ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama chini
ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambayo
inatembelea Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kuzungumza na watumishi wa
Mahakama na wadau mbalimbali na pia kutoa elimu kuhusu kazi zake.
“Tutambue kwamba ziko sheria,
miongozo na taratibu zinazoongoza vyombo vya upelelezi kwa lengo la kuwezesha
upelelezi kufanyika kwa wakati, weledi na ufanisi mkubwa. Tuhuma za jinai
zisizo na ulazima wa kufikishwa mahakamani zichunguzwe kwanza na hatimaye
majalada ya upelelezi yawasilishwe ofisi za mashtaka kwa ajili ya uamuzi na
hatua za kimashataka,” amesema.
Akizungumza katika mkutano wa Tume
hiyo wakati akitoa maelezo mafupi kuhusu matarajio ya Mahakama kwa wadau, Jaji Kiongozi amesema kuwa Jeshi la Polisi,
TAKUKURU, Uhamiaji na TANAPA ni washirika na wadau muhimu wa Mahakama katika
kutekeleza jukumu lake la msingi la utendaji kazi ambapo umuhimu wao huonekana
katika nyanja kadhaa, ikiwemo uanzishwaji wa mashitaka mahakamani na upelelezi
wa makosa ya jinai.
“Changamoto kubwa inavyovikabili vyombo
hivi ni ucheleweshaji wa kukamilika kwa kwa upelelezi. Changamoto imepelekea
matokeo hasi kama vile kuchelewa kumalizika kwa mashauri husika mahakamani,
mahabusu katika mashauri yasiyokuwa na dhamana kukaa magerezani kwa muda mrefu,
kuongezeka kwa msongamano magerezani na gharama kubwa ya kuwatunza mahabusu
magerezani,”alisema.
Amebainisha kuwa hivi karibuni
Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (Criminal Procedure Act) imefanyiwa
marekebisho kupitia mabadiliko ya sheria (Writen Laws (Misc. Amendments) Act
No. 1 of 2022) ambayo ni muhimu, mabadiliko ambayo yakizingatiwa na wadau hasa
vyombo vya upelelezi yatakuwa mwarobaini wa baadhi ya changamoto
alizozianinisha.
Mhe. Siyani ametaja baadhi ya maeneo
yanayogusa marekebisho hayo ikiwemo Kifungu cha 4 ambacho kimeongezewa kifungu
kidogo cha 3 ambacho kinaeleza kwamba pale ambapo tuhuma inajumuisha taswira ya
madai, kiutawala au jinai ni budi nafuu itolewayo kwa njia ya shauri la madai
au taratibu za kiutawala zitekelzwe kwanza kabla ya ufunguaji wa shauri la
jinai.
Amesema pia Kifungu cha 91(1) kimefanyiwa
mabadiliko na kubainisha kwamba pale ambapo upande wa mashtaka utaondoa shauri
kwa nolle prosequi, mshitakiwa hataweza kukamatwa na kushitakiwa tena kwa kosa
lilelile, isipokuwa tu kama kuna ushahidi wa kutosha dhidi yake na usikilizaji
wa shauri utaanza mara moja.
Kufuatia mabadiliko hayo, Jaji
Kiongozi amevishauri vyombo vya upelelezi kutumia njia za kisanyansi kukusanya
ushahidi thabiti ili kwenda na maendeleo ya karne ya 21, huku akitolea mfano wa
matumizi ya ushahidi wa vinasaba vilivyochukuliwa eneo la tukio, utambuzi wa
kisayansi wa vielelezo vinavyohusika na makosa ya jinai na huduma inayotolewa
na Forensic Bureau Dar es Salaam.
“Sheria imejenga mfumo thabiti
katika kushughulikia changamoto zinazotukabili, hasa mlundikano wa mashauri
mahakamani na ucheleweshaji wa mchakato wa utoaji haki, changamoto ambazo kwa
sehemu kubwa husababishwa na kuchelewa kukamika kwa upelelezi. Tatizo hili
litatatuliwa kwa utashi wa kila mmoja wenu kuzingatia sheria na taratibu
zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yenu,” alishauri Mhe. Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza katika mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali katika mnyororo wa utoaji haki leo tarehe 20 Juni, 2022 mjini Mtwara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni