Na Faustine Kapama– Mahakama, Lindi
Ziara ya Tume ya Utumishi wa
Mahakama katika Ukanda ya Kusini mwa Tanzania imeingia siku ya pili ambapo leo
tarehe 21 Juni, 2022 imetembelea Mkoa wa Lindi kuzungumza na watumishi na wadau
na Kamati za Maadili, hatua ambayo imeleta neema kwa wananchi katika Mkoa huo,
hususani ujenzi wa majengo ya kisasa ya Mahakama kwa ngazi zote.
Tume hiyo chini ya Mwenyekiti wake,
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma imeanza kwa kukutana na
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack
ambaye aliwakaribisha Makamishna na wajumbe wote na kuwaeleza fursa lukuki
zinazopatikana katika eneo lake la utawala.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha
mkoani Lindi, karibuni sana. Niliambiwa angalau utalala Lindi leo, sasa
nimesikia kidogo kidogo kwamba hamlali. Mtaifahamu lini Lindi? Mgelala ili mjue
Lindi siyo porini. Lindi inafunguka, ina madini yote mnayoyajua isipokuwa
almasi na dhahabu. Kwa hiyo ni fursa pekee mkikaa Lindi ili kuona fursa
mbalimbali zilizopo,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume huyo alimshukuru
Mkuu wa Mkoa kwa kuitangaza vyema Lindi, hususani fursa zilizopo katika eneo
lake, hatua ambayo viongozi wa Mahakama wanapaswa kuiga katika kutangaza uboreshaji
mzuri wa huduma unaofanyika. Jaji Mkuu
amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa huyo kuwa Mahakama ya Tanzania itajenga Mahakama
Kuu ya kisasa ili kushughulikia migogoro itakayojitokeza kutokana na kukua kwa
uchumi Lindi.
Baada ya ukaribisho huo, wajumbe wa
Tume walielekea katika ukumbi maalumu uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya
kukutana na watumishi wa Mahakama Lindi, wajumbe wa Kamati za Maadili za Mkoa
na Wilaya na baadaye wadau mbalimbali katika mnyororo wa utoaji haki. Katika
mikutano hiyo, viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya walipata nafasi ya kutoa
maoni yao na ushauri wenye lengo la kuboresha huduma za utoaji haki kwa
wananchi.
Wakuu wote wa Wilaya ndani ya Mkoa
wa Lindi wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma za utoaji
haki ikiwemo kujenga miundombinu ya majengo ya kisasa na pia matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika shughuli mbalimbali za
kimahakama. Viongozi hao wakashauri pia uwezekano wa kujenga nyumba za makazi
kwa Mahakimu ambao wamewaelezea kuwa wanafanya kazi nzuri katika maeneo yao.
Katika mikutano hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Mtwara, Mhe. Zainab Mruke alipata nafasi ya kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa
na wajumbe na kubainisha kuwa kwa sasa kuna majengo kadhaa ya Mahakama ndani ya
Mkoa huo yanayojengwa na mengine yataanza kujengwa kuanzia mwaka wa fedha
ujao, yaani kuanzia Julai, 2022.
“Mahakama inafanya uboreshaji mkubwa
sana, nchi ni kubwa na mahitaji ni mengi. Hivyo tunachofanya tunagawa kidogo
kidogo,”alisema. Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, ambaye pia ni Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alikata kiu ya wajumbe
alipotangaza kuwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kitajengwa Lindi kuanzia mwaka
wa fedha ujao, taarifa ambayo ilipokelewa kwa makofi na furaha.
Baada ya kufanya mikutano hiyo,
ujumbe wa Tume ulielekea katika eneo ambalo kuna jengo la kisasa la Mahakama ya
Hakimu Mkazi Lindi, ambalo limekamilika na muda wowote litakabidhiwa kwa
viongozi wa Mahakama kwa ajili ya kuanza kutumika.
Tume ya
Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania chini ya Ibara ya 112 kwa lengo la kusimamia mambo muhimu yanayohusu
Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania
(Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja wa Mahakama ya Rufani
anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe
wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ndiye Katibu wa Tume hiyo. Baadhi ya kazi za Tume hiyo ni
pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu,
kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu, mishahara na maslahi ya Majaji na
kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na kusimamia nidhamu yao.
Sehemu ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika mkutano huo. Kutoka kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Eliamini Laitaika, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mh. Sharmillah Sarwatt, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha.
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Zainab Mruke. Kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe . Dkt. Jaji Eliezer Mbuki Feleshi na Mawakili wa Kujitegemea Waandamizi, Mhe. Jenoveva Kato na Kalolo Bundala.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni