Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma amewataka wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama kusimamia
kikamilifu maadili kwa kuwa kamati hizo zina umuhimu mkubwa katika utawala wa
sheria na uhuru wa Mahakama.
Akizungumza
na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama wa Mkoa wa Mtwara pamoja
na Wilaya zake katika ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama iliyoanza mkoani humo,
Prof. Juma amesema Mahakama haiwezi kuwa na uhuru na nguvu endapo itakuwa
ikikumbana na changamoto za kimaadili.
“Tukiondoa
changamoto za kimaadili tutaweza kuimarisha uhuru wa Mahakama na kutoa uamuzi
unaoheshimika na wananchi katika mashauri mbalimbali yanayofikishwa
mahakamani”, alisema Mwenyekiti wa Tume.
Mwenyekiti
huyo amewataka wajumbe wa Kamati hizo kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao
umuhimu wa Kamati za Maadili ili wazifahamu na kuzitumia katika kuwasilisha
malalamiko yao ili waweze kupata haki zao za msingi. Aidha amewaomba wajumbe
hao pia kusimamia maadili ya wadau wengine katika sekta ya sheria na Mahakama
ambao wako katika mnyororo wa utoaji haki.
Mwenyekiti
huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema kunapokuwa na changamoto za
ukiukwaji wa maadili wananchi kuihukumu Mahakama kwa kuwa ndicho chombo chenye
jukumu la msingi la kusimamia mnyororo wa utoaji haki hivyo ni vema wadau
wengine wa utoaji haki wakazingatia suala la maadili wanapotekeleza majukumu
yao.
“Haki
haianzii mahakamani, inaanzia tangu mwananchi anapotoa taarifa ya uhalifu
katika kituo cha polisi na endapo taarifa hiyo haitatolewa kwa usahihi, ndiyo
mwanzo wa haki kutotendeka”, alisema Mwenyekiti huyo.
Awali
akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Prof.
Juma aliwapongeza watumishi hao kwa kuendelea kutoa huduma bora na kuwezesha kupungua
kwa malalamiko dhidi ya rushwa.
Alisema
kwa mujibu wa taarifa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini,
idadi ya malalamiko hayo imepungua. Aliongeza kuwa kupungua kwa malalamiko
yanayohusiana na rushwa kunaonesha kuwa hali ya kimaadili kwa watumishi wa
Mahakama imeimarika.
Naye Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama,
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani amewashauri
Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kutumia majukwaa waliyonayo kuwaelimisha
wananchi kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili na namna ya kuzitumia kuwasilisha
malalamiko yao dhidi ya vitendo vilivyo kinyume na maadili ya Maafisa wa
Mahakama.
“Viongozi
hawa katika ngazi za mikoa na wilaya wanapopata fursa ya kuzungumzia ajenda za
kitaifa kama vile Sensa, anuani za makazi na kadhalika, tunawaomba pia watumie
fursa hiyo kutoa elimu kuhusu Kamati za Maadili,” alisisitiza Kamishna
huyo.
Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mhe. Dkt. Elieza Feleshi ameishauri Mahakama ya Tanzania kuendelea na
mpango wake maalumu wa kujenga maadili kwa wanafunzi wa shule za sekondari na
vyuo vya elimu ya juu wanaosoma fani ya sheria kwa lengo la kupata wanasheria
wenye maadili mema na viongozi waadilifu hapo baadaye.
Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na Wilaya wakiwa kwenye Mkutano wa Tume jana mkoani Mtwara. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mtwara Bw. Dunstan Kyobya.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Enziel Mtei (kulia) akiwa kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Utoaji haki jana mkoani Mtwara. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Eliamani Isaya Laltaika na katikati ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni