Na Faustine Kapama– Mahakama, Lindi
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amesema vyombo vya habari ni daraja
muhimu baina ya Mahakama na wananchi, hivyo vinapaswa kushiriki katika kujenga taswira chanya ya Mahakama
kwa kuuhabarisha umma kuhusu mambo mazuri yanayotokea mahakamani ili kukuza imani
ya wananchi.
Mhe. Siyani ameyasema hayo katika siku ya pili ya ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambayo leo tarehe 21 Juni 2022 imetembelea Mkoa wa Lindi kuzungumza na watumishi na wadau wa Mahakama.
“Vyombo vya Habari ni daraja muhimu
baina ya mahakama na wananchi. Msiishie kukosoa mambo yanapokwenda mrama,
lakini tusemeeni kwa kuyatangaza zaidi mazuri yanayofanywa na Mahakama zetu ili
kujenga na kukuza imani ya wananchi kwa vyombo hivi vya haki,” amesema.
Mhe.
Siyani amesema vyombo vya habari ni wadau wakubwa wa Mahakama na katika kutimiza
jukumu lake la kutoa haki, ni lazima wananchi inayowahudumia wawe na imani na chombo
hicho na wanapaswa kufahamu juhudi zinazofanywa na Mahakama katika kuboresha huduma
zake za kutoa haki.
Kwa mujibu wa Mhe. Siyani, vyombo
vya habari vina mchango wa kujenga taswira ya Mahakama kwa umma ambapo dhamira ya
vyombo hivyo kupitia kazi zao inaweza kujenga picha chanya au hasi kwa Mahakama.
Aliotoa mfano kuwa kama vyombo vya habari
vitajikita kuandika mabaya pekee, imani ya wananchi itashuka na hilo likitokea
Mahakama itapoteza uhalali wa uwepo kwake na watu wataamua kujichukulia sheria
mkononi. Hakuna mtu atakayekuwa salama kuishi kwenye nchi ambayo watu wake
wanajikulia sheria mkononi,” ameonya Jaji Kiongozi.
“Kwa hiyo, bila kuathiri uhuru wa
vyombo hivi katika kutoa habari zinazofichua uovu kwa lengo la kurekebisha na
kuboresha, matarajio yetu pia kuwa vyombo vya habari vitatumia nafasi yake
kushiriki katika kujenga taswira chanya ya Mahakama kwa kuuhabarisha umma
kuhusu mambo mazuri yanayotokea mahakamani ili kukuza imani ya wananchi kwa
mahakama zao,” amesema.
Jaji Kiongozi pia alizungumzia
kuhusu Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka na wote wanaofanya kazi chini
yake wanapaswa kuongozwa na misingi iliyowekwa na Katiba ya nchi kupitia ibara
ya 59B (4) ambayo ni kutenda haki, kutokutumia madaraka vibaya, kuzingatia
maslahi ya umma. Amesema hayo ni mambo ambayo kila anayefanya kazi chini ya
ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka anapaswa kuyaishi.
“Mahakama
inatarajia kwamba ofisi ya Taifa ya Mashtaka itafanya kazi kwa kuzingatia misingi
hiyo na kama hilo litafanyika na kwa kuwa ofisi hii ndiyo inayosimamia upelelezi
wa makosa ya jinai, basi hakutakuwa na mlundikano wa mahabusu wa muda mrefu magerezani.
Aidha kukamilika kwa upelelezi ndani ya muda mfupi kutawezesha Mahakama pia
kusikiliza mashauri husika kwa kasi,” amesema.
Jaji
Kkongozi pia amewataja Afisa Huduma kwa Jamii kuwa ni mdau muhimu katika
kupendekeza adhabu mbadala kwa watuhumiwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo
adhabu husika ni chini ya miaka mitatu kama inavyobainishwa katika kifungu 3(1)
(4) cha Sheria (the Community Services Act (Cap. 291 R.E. 2019).
Amesema
maafisa huduma kwa jamii wana jukumu la kuwasilisha uchunguzi wa kijamii wa
watuhumiwa ambao wanastahili adhabu mbadala kwa makosa ya jinai kabla ya adhabu
husika kutolewa kwa mujibu wa kifungu 3(1)(4) cha Sheria (the Community
Services Act (Cap. 291 R.E. 2002).
Sehemu ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika mkutano huo. Kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume, Prof. Elisante Ole Gabriel, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Eliamini Laitaika, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mh. Sharmillah Sarwatt, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni