Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama
wakiwemo Mahakimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii wakati Serikali ikiendelea
kushughulikia maslahi yao pamoja na ya watumishi wengine wa Umma.
Akizungumza
na Watumishi wa Mahakama jana mkoani Lindi, Jaji Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema maslahi ya Mahakimu pamoja na watumishi
wengine wa Mahakama hayana budi kufanyiwa uboreshaji kutokana na majukumu
mazito waliyonayo ambayo hayaendani na kiwango cha mishahara wanachopata.
Akisisitiza
suala la nyongeza ya mishahara kwa Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa
Mahakama, Jaji Mkuu akitolea mfano wa Tume ya Jaji Warioba ya rushwa, alisema Tume
hiyo katika ripoti yake ya mwaka 1996 kwenye moja ya mapendekezo yake iligusia
suala la maslahi madogo kwa Mahakimu.
Kuhusu
suala la maadili kwa Mahakimu, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
alitoa rai kwa wenyeviti wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya
mkoa na wilaya kusimamia maadili ya Mahakimu na kuwaelimisha wananchi kuhusu
uwepo wa Kamati hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Lindi Bibi Zainabu Talack ameiomba Mahakama ya Tanzania
kuongeza idadi ya Mahakimu katika mkoa huo kwa kuwa waliopo hivi sasa hawatoshi
hali inayosababisha Hakimu moja kuhudumia Mahakama zaidi ya moja.
Kuhusu
maslahi ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu, Mkuu huyo wa mkoa alisema
kuwa Mahakama haina budi kuwawezesha watumishi hao ili waweze kutekeleza
majukumu yao kwa ufasaha.
Aliwataka
Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Umma kutumia fursa zilizopo mkoani humo
kujipatia kipato cha ziada baada ya saa za kazi.
“Mahakimu
wajishughulishe na shughuli za uzalishaji ili wawe na ustawi mzuri utakaowawezesha
kufanya kazi zao vizuri”, alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Tume
ya utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara yake yenye lengo la kujitangaza na
kuimarisha Kamati za maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya
katika mikoa ya Lindi na Ruvuma.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Ibrahim Hamis Juma akisikiliza hoja za Watumishi wa Mahakama mkoa wa Lindi wakati wa ziara ya Wajumbe wa Tume hiyo mkoani humo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Zainabu Muruke na kulia ni Katibu wa Tume na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bi. Zainabu Talack akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani Lindi.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama mkoa wa Lindi wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama mkoa wa Lindi wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni