Na. Emmanuel Oguda – Shinyanga
Mahakama Mkoa wa Shinyanga imetekeleza agizo la Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani kwa Mahakimu Wafawidhi
wa Mikoa yote kuendesha mafunzo kuhusu maadili kwa Mahakimu wote nchini walio
chini yao ili kutekeleza moja kati ya nguzo tatu zilizopo katika Mpango Mkakati
wa Mahakama wa Miaka Mitano ili kutoa haki kwa wakati kwa wananchi..
Hatua hiyo inafautia uamuzi wa Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga, Mhe Mary Mrio kuendesha mafunzo hayo katika
maeneo tofauti tofauti kwa Mahakimu wote mkoani hapa kutoka Mahakama ya Hakimu
Mkazi Shinyanga, Mahakama ya Wilaya Shinyanga, Mahakama ya Wilaya Kishapu na
Mahakama ya Wilaya Kahama.
Akihitimisha mafunzo hayo alipokuwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Kishapu, Mhe Mrio aliwahimiza Mahakimu wote kuwa waadilifu wanapotekeleza
majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi pasipo huba, chuki wala upendeleo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo alisema Mahakimu wote ndani
ya Mkoa wa Shinyanga wanatakiwa kuzingatia Tangazo la Serikali (GN.1001/2020) linalowataka
kuzingatia mambo muhimu, hususani kuwa Huru, Kutopendelea, Mgongano wa
kimaslahi, Uadilifu, Usawa, Umahiri na Uaminifu (Independence, Impartiality,
Conflict of interest, Integrity, Equality, Competence and Deligence’’).
Mhe. Mrio alisema hatakubali kuona Hakimu yoyote
anakiuka maadili katika kutekeleza majukumu yake na kutotenda haki kwa wananchi
kinyume na kiapo chake. Aidha, aliwataka
Mahakimu kutojihusisha na vitendo ya rushwa wakati wote kwani kufanya hivyo ni
kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
“Mahakama ya Tanzania haiko tayari kufumbia macho
masuala ya rushwa kwa Mahakimu na watumishi wote ndani ya Mhimili huu wa utoaji
haki nchini,” alisema mwishoni mwa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mahakama ya
Tanzania chini ya Mpango wa Mafunzo (Training Policy 2019) kwa watumishi wake.
Kwa upande wao, Mahakimu waliopata mafunzo wameahidi kuzingatia
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021 –
2024/2025 pamoja na maagizo yake ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi
sambamba na kuzingatia maadili katika majukumu yao ya kila siku.
Aidha Mahakimu hao wameahidi kuwa Mahakama za Mkoa wa
Shinyanga zitakuwa mfano wa kuigwa katika kutoaji haki kwa wakati kufuatia
shindano lililoanzishwa hivi karibuni na Mahakama ya Tanzania kutafuata
Mahakama inayotoa huduma bora kwa wananchi (Court of Excellence Perfomance).
Mapema mwezi Machi, 2022 Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe Athumani Matuma aliwataka Mahakimu na watumishi
wote kuhakikisha Kanda hiyo inaibuka mshindi katika kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Shinyanga, Mhe. Mary Mrio (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Wilaya ya
Shinyanga baada ya mafunzo kuhusu maadili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni