Jumanne, 7 Juni 2022

WAKALA WA MAJENGO WAKABIDHI NYUMBA MAKAZI YA JAJI MFAWIDHI TABORA

Na Amani Mtinangi- Mahakama Kuu Tabora

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeikabidhi Mahakama ya Tanzania jengo la gorofa moja na la kisasa kwa ajili ya makazi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora.

Hafla ya kukabidhi jengo hilo ambalo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 525 za Kitanzania ilifanyika hivi karibuni mjini hapa mara baada ya kukamilika kwa mradi ambao umetekelezwa kwa takriban  miaka 10.

Kaimu Meneja wa TBA mkoani Tabora, Bw. Abraham Ndazi alikabidhi jengo hilo kwa niaba ya uongozi wa Wakala wa Majengo nchini kwa Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Nashon alisema kuwa licha ya kumwezesha Jaji Mfawidhi kuishi katika makazi bora na salama, jengo hilo jipya lenye vyumba vitatu pia litapunguza gharama za matumizi ya ofisi.

Bw. Nashon  ambaye alipokea jengo hilo kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania alisema kuwa Mahakama imekuwa ikitumia fedha nyingi kulipia pango la nyumba ya makazi ya Jaji Mfawidhi.

Amesema kiasi cha shilingi milioni 14 za Kitanzania zimelipwa, sawa na shiingi 1,180,000/= kwa mwaka. Bw. Nashon ameupongeza uongozi wa TBA Mkoa wa Tabora kwa kazi nzuri waliyoifanya ya ujenzi hadi kukamilika kwa mradi huo.

Naye Kaimu Meneja wa Mkoa wa Tabora aliishukuru Mahakama Kuu Tabora kwa namna wanavyoshirikiana kutekeleza miradi inayosimamiwa na Wakala na kuahidi kuendeleza ushirikiano na Mahakama katika kutekeleza mjukumu yake.

Jengo lenyewe upande wa mbele.

Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda Nashon (kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa Kaimu Meneja wa TBA Tabora, Bw. Abraham Ndazi wakati wa makabidhiano ya jengo la makazi ya Jaji Mfawidhi lililogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi 525.

Muonekano wa mbele wa jengo la makazi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora. 
Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Tabora akiambatana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora, Mhe. Gabriel Ngaeje pamoja na baadhi ya maafisa na watumishi wa Mahakama kukagua jengo hilo wakati wa makabidhiano.

Picha ya pamoja baada ya makabidhiano.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni