Na Emmanuel Oguda – Shinyanga.
Timu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, mpira wa
miguu wanaume (Mahakama FC), jana ilitoana jasho na timu ya Veterani ya Mjini
Kahama (Kahama Veterani) na kupoteza mchezo huo kwa taaabu kwa kufungwa magoli
2 -1.
Mchezo huo wa kirafiki wa kisisimua ulishuhudiwa na Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athumani Matuma. Kipindi
cha kwanza kilianza kwa kasi huku Mahakama FC ikisakata kabumbu kwa uhakika na kulisakama lango la wapinzani wao mara kwa
mara.
Hata hivyo, katika dakika ya 25 ya kipindi hicho, Kahama Veterani wakafanikiwa
kupata bao kupitia mshambuliaji wao Denis Deocles. Baada ya kupachikwa bao
hilo, Mahakama FC wakacharuka na kulishambilia lango la wapinzani wao kama
nyuki.
Katika dakika ya 33 Mahakama FC waliweza kusawazisha goli hilo
kupitia mshambuliaji wake machachari Patrick Mluge ambaye aliweka kimyani bao safi
baada ya kupokea pasi mpenyezo kutoka kwa winga, hivyo hadi dakika 45 za
kipindi cha kwanza zinakamilika timu zote mbili zilikuwa zimetoshana nguvu kwa
kufungana goli 1 - 1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo timu zote mbili
zilionyesha uwezo mkubwa katika kushambuliana kwa zamu. Hata hivyo, katika dakika
ya 77 ya kipindi hicho, mshambuliaji wa Kahama Veterani Miraji Kasimu aliachia
shuti kali kwenye lango la Mahakama FC lililomshinda golikipa Novat Mgongolwa
na kuandika bao la pili.
Katika dakika ya 85, Mahakama FC wakapata nafasi adhimu baada ya
mchezaji wa Kahama Veterani kucheza faulo nje ya 18, nafasi ambayo Mahakama FC
wakaipoteza. Hadi dakika 90 za mchezo zinakamilika Kahama Veterani waliibuka
washindi dhidi ya Mahakama FC kwa kufunga mabao 2 – 1.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Mahakama FC,
Abdulmuuminu Mbaraka amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi na
kujiimarisha na ameona makosa kadhaa ambayo ameahidi kuyafanyia kazi na kikosi
chake kuendelea kuwa imara na thabiti wakati wote.
Awali akifungua mchezo huo uliochezwa ndani ya dimba la CCM
Kambarage katika Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Matuma aliwapongeza wanamichezo
hao kwa kuandaa mchezo wa kirafiki kwani michezo ni afya, hujenga afya ya akili
na kuboresha mahusiano baina ya wanamichezo hao. Aliwataka wanamichezo hao
kuendelea kufanya mazoezi ili kushiriki katika michezo mbalimbali ndani ya
Kanda.
Naye mwakilishi wa wanamichezo kutoka timu ya Kahama Veterani
aliyefahamika kwa jina moja la Gwamaka, aliwashukuru viongozi wa Mahakama FC
kwa kuwaalika katika mchezo huo wa kirafiki ambao pia ni wa marudiano.
Alisema kuwa katika mchezo huo walikuwa wamejiandaa kulipa kikasi
baada ya Mahakama FC kuwazabua Kahama Veterani 1 – 0 katika mchezo wa kirafiki
uliopigwa Mjini Kahama mapema mwezi Machi mwaka huu.
Kapteni wa Mahakama FC Benedict Mtewa akitimiza wajibu wake ndani ya dimba la CCM Kambarage Shinyanga wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Kahama Veterani.
Wachezaji wa Mahakama FC ya Shinyanga wakipasha misuli kabla ya kuanza kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Kahama Veteran ya Mjini Kahama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni