Na Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Sports Ijumaa
tarehe 24 Juni, 2022 ilitoshana nguvu na Timu ya Vingunguti Veteran baada ya
kutoka sale ya 2-2 katika mechi nzuri ya kirafiki iliyochezwa kwenye Viwanja
vya Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law school) iliyoko Mikocheni jijini Dar es
Salaam.
Mchezo huo uliochezwa
kuanzia majira ya 10:20 jioni ulianza kwa kasi na iliwachukua dakika ya 16 tu katika
kipindi cha kwanza kwa Mahakama Sports kupachika bao zuri kupitia mshambuliaji
wake hatari Gulam Katwila baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa mshambuliaji machachari
King's Chilemba Hassan Chikawe.
Kupatikana kwa bao hilo
kuliamsha ari ya wachezaji wa Mahakama Sports ambao walilisakama lango la
wapinzani wao Vingunguti Veteran mara kwa mara ambapo kulikuwepo na kusa kosa
za hapa na pale.
Hata hivyo, Vingunguti
Veteran walijibu mashambulizi katika dakika ya 31 na kufanikiwa kupata bao,
hivyo kuufanya ubao wa matokeo kusomeka 1-1. Hadi kipindi cha kwanza kwa dakika
45 kinamalizika timu zote zilienda kwenye mapumziko zikiwa nguvu sawa.
Mchezo katika kipindi
cha pili ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu ambapo katika dakika ya
73 Mahakama Sports ikafanikiwa kupachika bao la pili lililofungwa kwa shuti
kali na Mshambuliaji machachari Chilemba Hassan Chikawe (King's Chikawe) baada
ya kupokea pasi murua kutoka kwa mlinzi wa kushoto Chentro.
Hata hivyo, baada ya
kosa kosa za hapa na pale kutoka timu zote mbili, Vingunguti Veteran walipata
bahati ya kusawazisha goli hilo majira ya jioooni kabisa katika dakika 87 ya
kipindi cha pili. Hadi mpira unamalizika Mahakama 2 na Vingunguti Veteran 2.
Alizungumza baada ya
mchezo huo, Kocha wa Mahakama Sports Spear Mbwembwe amewapongeza vijana wake
kwa mchezo mzuri waliouonyesha katika vipindi vyote na ameridhishwa na matokeao
hayo kwa kuzingatia ugumu na uzoefu wa timu waliyocheza nayo.
“Hii ilikuwa ni mechi
safi, nzuri na muhimu sana kwetu, ni mechi ya kujipima na kujiweka sawa. Kwani
Timu tuliyocheza nayo ni Timu nzuri yenye uwezo mkubwa kisoka. Vingunguti Veteran
ina wachezaji wazuri wanaojua mpira, ni wazoefu na wenye pasi za uhakika, ni
wachezaji wenye kasi sana hasa katika ushambuliaji,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Mahakama Sports Wilson Dede ameshukuru kwa timu yake kupata matokeo hayo na
ameona uwezo wa timu yake, ipo vizuri na inazidi kuimarika kwa kiasi
kinachoridhisha. Amesema bado wanaendelea na mazoezi ya kujinoa zaidi wakiwa chini
ya kocha mzoefu na mahiri Spear Dunia Mbwembwe ambaye ni kocha mchezaji, aliyekuwa golkipa wa zamani wa Timu ya Simba
Sports Club.
“Tunawaomba wanamichezo
wote na watumishi wengine wa Mahakama Mikoa yote, wajitokeze na kushiriki
kufanya mazoezi ya pamoja kwa nia ya dhati ya kuendeleza michezo ndani ya
Mahakama, tuwe na nia ya kuimarisha timu yetu pamoja na kuimarisha afya zetu,”amesema.
Katika mechi hiyo wachezaji
wa Mahakama Sports walikuwa Shaibu Hassan Kanyochole, Chentro, Msimbe Banzi, Saidi
Albea, Jamali Mkumba, Victor, Ismail Lulambo, Gulam Katwila, Chilemba Hassan
Chikawe,Mohamed Pazi, Mohamed Shabani Ugomba na Charles Mwakapimba, huku benchi
la ufundi liliongozwa na Romwan Adam (Roma), Mariam Mayala na Jamila.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni