Na Lydia Churi- Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wadau mbalimbali wa Mahakama kujitengenezea
utaratibu wa kutangaza kanuni zao za maadili ili kuongeza uwazi na uwajibikaji
wa watumishi kwa wananchi katika mnyororo mzima wa utoaji haki.
Akizungumza
katika Mkutano wa Tume hiyo na wadau wa utoaji haki leo mjini Songea, Jaji Mkuu
alisema Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa wazi wa kushughulikia
maadili ya watumishi na kupokea malalamiko ya wananchi yanayohusiana na
maadili.
“Sisi
hatuogopi kukosolewa na hatusiti kupokea malalamiko kwa sababu malalamiko hayo
yanaweza kuleta kiu kwa wananchi ya kutaka kujua zaidi shughuli zinazofanywa na
Mahakama”, alisema Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu pia amewaomba wadau hao wa Mahakama kutangaza namna wanavyoshughulikia
malalamiko ya kimaadili yanayoelekezwa kwao na wananchi ili watanzania wengi
zaidi wafahamu na kuwasilisha malalamiko yao. Alisema, hatua itasaidia upatikanaji wa haki kwa
wakati.
Alisema
malalamiko dhidi ya Mahakama hutokana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na
wadau wa Mahakama. Alisema kwa mfano malalamiko dhidi ya Madalali wa Mahakama,
ni rahisi kwa mwananchi wa kawaida kujua kuwa yanatokana na Mahakama wakati
kiuhalisia malalamiko hayo hutokana na kazi zinazofanywa na wadau.
Aidha,
Jaji Mkuu pia amewataka wadau wa utoaji haki nchini kutangaza utayari wao wa
kupokea malalamiko yanayohusu maadili yasiyofaa kwa watumishi wanaofanya kazi
na Taasisi za wadau wa Mahakama wakiwemo Polisi, Magereza, Waendesha Mashtaka,
Mawakili wa kujitegemea pamoja na wadau wengine.
Akizungumzia
Mawakili, Jaji Mkuu alisema hivi sasa kuna mabadiliko ya sheria yaliyoruhusu
Mawakili kuanza kutumika katika Mahakama za Mwanzo nchini hivyo aliwataka wadau
kuhakikisha Mawakili hao wanakuwa waadilifu kwa kuwa Mahakama hizo zinabeba
asilimia 70 ya mashauri yote.
“Chama
cha Wanasheria nchini (Tanganyika Law Society) kianze sasa kushughulikia
maadili ya Mawakili wao wenyewe bila vyombo vingine kuwaingilia”, alisisitiza Jaji
Mkuu.
Wajumbe
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wamemaliza ziara yao yenye lengo la kuitangaza
Tume na kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili katika mikoa ya Mtwara,
Lindi na Ruvuma. Katika ziara hiyo, Wajumbe hao walikutana na wajumbe wa Kamati
za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mikoa na wilaya pamoja na wadau wa
utoaji haki nchini.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye
katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha
Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ya Utumishi wa
Mahakama ni chombo cha Kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa
Mahakama ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama/Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na wadau wa utoaji haki mwishoni mwa wiki mjini Songea wakati wa Mkutano wa Tume na wadau hao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni