Na Faustine Kapama– Mahakama, Songea
Tume ya Utumishi wa
Mahakama leo tarehe 23 Juni, 2022 imemaliza ziara yake katika mikoa ya Kanda ya
Kusini mwa Tanzania kwa kuzungumza na kutoa elimu kuhusu kazi zake kwa watumishi
wa Mahakama, wadau mbalimbali katika mnyororo wa utoji haki na Wenyeviti wa
Kamati za Maadili wa ngazi katika Mkoa na Wilaya kwa kutembelea Mkoa wa Ruvuma.
Chini ya Mwenyekiti
wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Tume hiyo ilianza
kwa kukutana na Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Wilbert Ibughe na kufanya naye
mazumgumzo mafupi kabla ya kuelekea kwenye ukumbi maalumu ambao ulikuwa
umeandaliwa kwa ajili ya kufanya mikutano na wadau mbalimbali.
Katika mikutano hiyo, Mkuu
wa Mkoa huyo ameahidi kushirikiana na Mahakama ikiwemo kutoa kipaumbele kwenye
mahitaji yake ya kupata viwanja kwa ajili ya makazi ya Mahakimu ili kuuwezesha
Mhimili huo wa dola kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na ufanisi unaohitajika.
Kikao cha kwanza
kiliwahusisha wadau mbalimbali wa Mahakama wakiwemo Jeshi la Polisi, Magereza,
Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, Viongozi wa dini, Maafisa Ustawi
wa Jamii pamoja na wadau wengine katika mnyororo wa utoaji haki. Baada ya hapo,
ulifuata mkutano wa Wenyeviti wa Kamati za Wilaya na Mkoa kabla ya wajumbe wa
Tume hiyo kukutana na watumishi wa Mahakama katika Mkoa wa Ruvuma.
Kabla ya vikao vyote
hivyo vitatu ambavyo viliongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania kama Mwenyekiti wa
Tume kufanyika, washiriki wote walipata burudani safi kutoka kwa Kwaya kabambe
ya Mahakama, Kanda ya Songea ambayo iliatumbuza kwa nyimbo mbalimbali, hususani
ule unaohamasisha wananchi kushiriki kwenye sensa, wimbo ambao ulionyesha
kukonga nyoyo za maafisa na wadau wote waliohudhuria mikutano hiyo.
Katika kikao cha mwisho
cha watumishi wa Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe.
Yose Mlyambina aliwasilisha taarifa ya utendaji wa Mahakama katika Kanda yake
ambayo imesheheni mambo mbaloimbali ya kiutendaji.
Mhe. Mlyambina
amewaeleza Makamishna na wajumbe wa Tume, pamoja na mambe mengine, kuwa Mahakama
Kanda ya Songea wameendelea kusimamia nidhamu ya watumishi kwa kutoa elimu ya
maadili ya Mahakimu na utumishi wa Mahakama.
“Yapo makatazo
tuliyoyatoa kupitia vikao vyetu vya ndani na tumeendelea kuonyana na
kurekebishana kadiri tuwezavyo. Tumeunda kamati za nidhamu kuanzia ngazi ya
Kanda hadi wilaya kwa lengo la kurekebisha tabia za watumishi zinazokinzana na
maadili ya kiutumishi,” amesema.
Mhe. Mlyambina ameeleza
kuwa Kamati za maadili za maafisa wa Mahakama kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Wilaya
zinaendelea kutekeleza majukumu yake vizuri ambapo katika kipindi cha mwaka
2021/2022 kamati hizo zimekaa vikao vyote vinavyotakiwa kisheria na taarifa za
vikao hivyo zimewasilishwa.
“Aidha, Kanda ya Songea
ilitekeleza agizo la kuundwa kwa kamati za nidhamu za watumishi wasio mahakimu
kwa kuteua wajumbe na mwenyekiti ni mtumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mpaka sasa hakuna shauri lolote la nidhamu kwa mtumishi lililowasilishwa kwenye
kamati hiyo,” amesema.
Akizungumzia hali ya
mashauri, Jaji Mfawidhi huyo amebainisha kuwa
Mahakama Kanda ya Songea imeendelea kutekeleza jukumu la msingi na la
kikatiba la utoaji haki kwa wananchi kwa Mahakama kupokea, kusikiliza na kutoa
hukumu kwa mashauri mbalimbali yanayofikishwa mahakamani kuanzia ngazi ya Mahakama
za Mwanzo hadi ngazi ya Mahakama Kuu Kanda ya Songea.
Amesema katika
usikilizaji wa mashauri kuanzia Januari hadi Juni, 2022, Mahakama Kuu Kanda ya
Songea na Mahakama za chini yake kwa mwezi Desemba 2021 kulikuwa na mashauri ya
madai 324 yaliyobaki na yakafunguliwa mashauri 930, mashauri 955 yalimalizika
na mashauri 299 yamebaki.
Mhe. Mlyambina amesema kuwa kwa upande wa mashauri ya jinai, kwa mwezi Desemba mashauri ya jinai 803 yalibaki, mashauri 1849 yalifunguliwa, mashauri 1992 yaliamuriwa na mashauri 632 yamebakia.
Meza kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Tume na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya Tume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni