Na Faustine Kapama– Mahakama, Songea
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amezishauri mamlaka
zinazosimamia uendeshaji wa Mabaraza ya Ardhi kutoa uwezeshaji wa kutosha ili
yaweze kutimiza majukumu yake kikamilifu kwani malalamiko yanayokuja mahakamani
kutokea kwenye taasisi hizo yanaichafua Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Siyani ameyasema
hayo katika siku ya mwisho ya ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya
Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambayo
leo tarehe 23 Juni 2022 imetembelea Mkoa wa Ruvuma kuzungumza na watumishi, wadau
mbalimbali wa Mahakama na Wenyeviti wa Kamati za Maadili kwa ngazi ya Mkoa na
Wilaya.
“Wizara na Mamlaka
zinazaosimamia Mabaraza hayo zinatakiwa kuyawezesha kufanya kazi kwa kuongeza
utendaji, kuwapa vitendea kazi na kusimamia nidhamu na uadilifu. Yapo maeneo
tumepita katika ziara hii, yupo Mwenyekiti mmoja anahudumia Mkoa mzima. Kwa hiyo
malalamiko yatakuja tu na malalamiko dhidi ya Mabaraza ni malalamiko ya
Mahakama,”amesema.
Akieleza matarajio ya
Mahakama kwa wadau mbalimbali katika myororo wa utoaji haki nchini, Mhe. Siyani
amesema kuwa Mabaraza ya Ardhi yamekuwa ni sehemu ya malalamiko yanayopokelewa
dhidi ya Mahakama na kwamba wananchi hawajui tofauti kati ya Baraza la Ardhi na
Mahakama.
“Kwa hiyo, asipotendewa
haki analalamika dhidi ya Mahakama na msingi wa malalamiko hayo ni lile takwa
la kikatiba kwamba Mahakama ndiyo iliyopewa kauli ya mwisho ya kutoa haki. Kwa
hiyo, akiona katendewa ndivyo sivyo anajua Mahakama ndiyo ambayo haijamtendea
haki,” amesema.
Kwa mujibu wa Jaji
Kiongozi, kwa sasa Mahakama haiwezi kuwa mbali na malalamiko hayo na kama
Mabaraza ya Ardhi hayataimarishwa na utendaji wake kupimwa hali hiyo
itaendelea.
Akaeleza matarajio ya
Mahakama kwa mdau huyo kuwa Mabaraza hayo hayatakwamisha kasi ya usikilizaji wa
rufaa na mapitio ya mashauri ya migogoro ya ardhi kwa kuhakikisha kumbukumbu au
majalada ya mashauri hayo yanawasilishwa haraka iwezekanavyo katika Mahakama
Kuu yanapoitishwa.
Kwa upande wa wananchi, Mhe.
Siyani amebainisha kuwa Mahakama inatarajia kwa mdau huyo ambaye pia ni muhimu kushiriki
uboreshaji unaoendelea kwa kuacha kushawishi rushwa kwa watumishi wa Mahakama
na hata wao wakiombwa kukataa kutoa rushwa na badala yake watoe taarifa za
kweli kwenye mamlaka husika kuhusu vitendo hivyo vya ukosefu wa maadili.
Amewaomba wananchi kuondokana
na hisia za rushwa hata kama hawajaombwa na hata kama mazingira kuwa yameboreshwa
na hakuna rushwa, lakini bado baadhi yao wanafikiri hawawezi kupata huduma
mahakamani bila kutoa rushwa.
“Kazi kubwa
imeshafanyika sasa hivi na niwaombe wananchi na wadau wote kuanza kuondokana na
dhana kwamba huwezi kupata haki mahakamani mpaka utoe rushwa, tumehama huko,
hatuko tena. Tunataka kuwa na taasisi ambayo hainyoshewi vidole. Hatutaki kuwa
miongoni mwa taasisi ambazo zinahusishwa na ukosefu wa maadili,” alisema.
Jaji Kiongozi
aliwageukia Mawakili wa Kujitegemea kwa kuwataka kuacha kutumia mbinu za
kiufundi kama mapingamizi ya awali wakati wa kusikiliza mashauri katika
Mahakama za Mwanzo, hatua ambayo itasababisha ucheleweshaji, hivyo kuwanyima
wananchi kupata haki zao kwa wakati.
Amebainisha kuwa kufuatia
marekebisho ya sheria, sasa hivi Mawakili wanaruhusiwa kutoa huduma kwenye
Mahakama za Mwanzo hapa nchini, lakini changamoto ambayo imejitokeza ni kuona wanakwenda
katika Mahakama hizo katika mwendo ule ule walionao kwenye Mahakama zingine
walizokuwa wanahudumu kuanzia Mahakama za Wilaya mpaka Mahakama Kuu.
“Matokeo yake ni kwamba
mbinu za kiufundi zinatumika sana katika Mahakama za Mwanzo. Hizi Mahakama kama
mlivyomsikia Jaji Mkuu zinapokea zaidi ya asilimia 70 ya mashauri yote katika
nchi yetu. Msingi mkubwa katika Mahakama hizi ni mapatano katika kufikia haki.
Ni matarajio ya Mahakama kuwa uwepo wa Mawakili usiondoe dhana hiyo ya kupatana
kwa kutumia zaidi mbinu za kiufundi,” amesema.
Amesema kuwa Mawakili wanatarajiwa kuonyesha weledi wao na kutumia misingi ya kupatana na maridhiano
baina ya wadaawa, hivyo ni matarajio ya Mahakama kuwa uwepo wa Mawakili kwenye Mahakama hizo hautaathiri kasi ya
usikilizaji wa mashauri.
Kadhalika Jaji Kiongozi amesema
Mawakili wanatarajiwa kuwa chachu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) ambapo Mwenyekiti wa Tume amekuwa akiwapokea Mawakili mara mbili kila
mwaka, lakini bado hawajaonyesha mwamko wa moja kwa moja kupokea hizo kauli za
matumizi ya teknilojia.
“Hivyo nitoe wito kwa
Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kushiriki moja kwa moja katika jitihada za
Mahakama kuelekea matumizi kamili ya teknolojia katika usikilizaji wa mashauri. TLS iwajengee uwezo wanachama wake
kutumia njia hii na sisi tupo tayari kushirikiana nao kuhakikisha kwamba
Mawakili wanakuwa chachu ya uboreshaji katika Mahakama ya Tanzania,” amesema.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akichagiza jambo.
Meza kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Tume na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikifuatilia masuala mbalimbali katika mkutano huo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. Yose Mlyambina na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.Sehemu ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika mkutano huo. Kutoka kushoto ni, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mh. Sharmillah Sarwatt, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha.
Makamishna wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama wakiwa katika mkutano huo. Kutoka kulia ni Jaji wa
Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, na Mawakili wa Kujitegemea Waandamizi, Mhe.
Jenoveva Kato na Kalolo Bundala na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na
Katibu wa Tume, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni