Alhamisi, 30 Juni 2022

MAHAKAMA YA TANZANIA YASIKILIZA NA KUAMUA MASHAURI KWA ASILIMIA 100

Na Magreth Kinabo- Mahakama 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mahakama ya Tanzania imefanya kazi kubwa ya kusikiliza na kuamua mashauri kwa asilimia 100 kwa kipindi cha mwaka 2021. 

 Akizungumza jana wakati taarifa yake na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kwenye mkutano wa Baraza la Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama hiyo, wa siku mbili unaofanyika kwenye ukumbi LAPF, ambapo alisema mashauri hayo ni pamoja na yale ya zamani ambayo yamekuwa ni chanzo cha malalamiko na kupoteza imani kwa wananchi.

 “Hadi kufika Desemba mwaka 2020, mashauri 62,470 yalibaki katika ngazi zote za Mahakama. Katika kipindi cha mwaka 2021 jumla ya mashauri 232,280 yalifunguliwa na mashauri 230,749 yalisikilizwa sawa na asilimia 100 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika kipindi hicho,” alisema Prof. Gabriel.

 Aliongeza kwamba mashauri yaliyobaki mahakamani mwaka 2021 ni 64,001. Mashauri ya mlundikano (backlog) ni 6,994 sawa na asilimia 10.9 ya mashauri yote yaliyobaki. Alisema katika kipindi cha mwaka, 2021, wastani wa mzigo wa kazi kwa kila Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani ni mashauri 917.
 Kwa kila Jaji wa Mahakama Kuu ni mashauri 411. Mahakimu katika Mahakama za Hakimu Mkazi ni 194, Mahakama za Wilaya ni 196 na Mahakama za Mwanzo ni 193. Alifafanua kwamba muhimu ni mafanikio makubwa yaliyopatikana katika upunguzaji wa mashauri ya zamani kwenye ngazi ya Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Mahakama za chini yaliyokuwa na umri zaidi ya miaka 5 “Uimarishwaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) umesaidia kusikiliza Mashauri mengi kwa muda mfupi na kuokoa kiwango kikubwa cha fedha. Kwa mfano, mwaka 2021 jumla ya mashauri 17,979 yalisikilizwa kwa njia ya mtandao na hivyo kuokoa kiasi cha shilingi 2,750,092,736,’’ alisisitiza. 

 Mtendaji huyo alisema changamoto pekee inayoikabili Mahakama na iliyobaki ndani ya uwezo mhimili huo ni usimamizi na ufuatiliaji wa Mahakama za chini ili kuhakikisha nyenzo hiyo muhimu inatumika ipasavyo. Kwa kuwa inasaidia kukabiliana na ufinyu wa bajeti na uhaba wa watumishi uliopo. 

Alisema Mahakama katika kipindi cha mwaka 2021/22 imefanikiwa kutoa kompyuta mpakato 161 kwa mahakimu wote ikiwa ni nyenzo muhimu katika uandaaji wa hukumu. 

Hivyo ni imani yake kuwa vifaa hivi muhimu vitaokoa muda na kutoa huduma kwa wakati. Mahakama imeendelea na utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama, ambapo katika mwaka 2021/2022 miradi 60 inatekelezwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama. Hadi kufikia mwisho wa robo ya tatu kwa tarehe 31 Machi, 2022 Mahakama ilikuwa na jumla ya watumishi 5,808. 

Kati yao 26 ni Majaji wa Mahakama ya Rufani, 80 ni Majaji wa Mahakama Kuu, 1,118 ni Mahakimu Wakazi, 261 ni Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na 4,424 ni Watumishi wa Kada zingine mbalimbali. 

Hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya lazima ya watumishi 10,352, sasa Mahakama ina uhaba wa watumishi 4,544. Aidha watumishi 2,096 waliidhinishwa kupandishwa vyeo mwezi Mei, 2021.Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Mahakamaninaendelea na zoezi la kupandisha vyeo watumishi 957.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni