Na Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya Tanzania imepewa tuzo maalum na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (UTUMISHI) kwa kushinda nafasi ya pili (2) kati ya Idara Zinazojitegemea 26 kwa utendaji mzuri katika usimamizi wa rasilimaliwatu kwa kufuata Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021/2022.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi tuzo hiyo kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama leo tarehe 02 Juni, 2022, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu- Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amesema kuwa tuzo hiyo ilitolewa katika kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wote kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Mikoa; Majiji, Miji na Halmashauri, Taasisi za Serikali kama Vyuo, Vyuo Vikuu na Mashirika ya Umma kilichofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
“Mhe. Mtendaji Mkuu nipo hapa leo kwa ajili ya kukabidhi tuzo maalum iliyotolewa kwa Mahakama katika kikao ambacho uliniagiza na kunipa ruhusa ya kuhudhuria, katika kikao hiki Mgeni Rasmi Mhe. Jenista Mhagama, Waziri-UTUMISHI alitoa tuzo kwa Taasisi za umma ambazo zimekuwa na utendaji mzuri, hivyo Mahakama ilifanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye kundi la Idara Zinazojitegemea baada ya Tume ya Uchaguzi kushika nafasi ya kwanza na Ofisi ya Bunge kuwa wa tatu,” amesema Bi. Beatrice.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa, utoaji wa Tuzo hizo umezingatia vigezo kadhaa ikiwemo; kutumia vema Mfumo wa Taarifa za Kumbukumbu na Mishahara ya Watumishi (HCMIS) na kuhamisha kwa mafanikio na kwa wakati taarifa za watumishi kutoka mfumo wa ‘Lawson’ kwenda Mfumo wa ‘HCMIS’ usahihi wa taarifa za watumishi katika Mfumo huo.
Ametaja vigezo vingine ni pamoja na; kupungua kwa idadi ya malalamiko ya watumishi yanayopelekwa UTUMISHI kupitia mfumo/utaratibu wa ‘e-mrejesho’ na uwepo wa malalamiko yaliyosajiliwa; kushughulikia ipasavyo na kutekeleza kwa wakati maelekezo na masuala mbalimbali ya kiutumishi yanayotolewa na UTUMISHI na haiba na utendaji kazi mzuri.
Kigezo kingine ni Uzingatiaji wa maadili na kushughulikia mashauri ya nidhamu kwa wakati na kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amekiri kufurahishwa na tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Kwetu sisi Mahakama, hii tuzo ni kitu kikubwa sana na tunathamini na hii itatupa nguvu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi ili wananchi waendelee kunufaika na huduma tunazozitoa,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (UTUMISHI) waandaaji wa Tuzo hizo, huku akipongeza hatua hiyo ya kutambua utendaji kazi bora na hivyo ameahidi kuwa, Mahakama itaendelea kufanya vizuri zaidi ili kushika nafasi ya kwanza, vilevile Mkuu huyo amewapongeza Watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania kwa kufanya kazi kwa kujituma hali iliyosababisha Mhimili huo kutambulika na kushika nafasi hiyo.
Aidha; Prof. Ole Gabriel amesema kuwa Mahakama ya Tanzania inaendelea kufanya maboresho mbalimbali yenye lengo la kuwafikia wananchi, ametoa wito kwa wananchi kutosita kutoa maoni, malalamiko na ushauri wowote kupitia nambari ya simu ya huduma kwa mteja ambayo ni 0752 500 400.
Dhumuni la kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kilichofanyika tarehe 26 na 27 Mei, 2022 ilikuwa ni kutathmini utendaji kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa wananchi na kutambua Taasisi ambazo zimekuwa zikionesha jitihada za wazi katika kuboresha utoaji huduma kwa umma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama, Bi. Beatrice Patrick wakifurahia tuzo hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni