Na Stanslaus Makendi-Mahakama, Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma,
Mhe. Gerson Mdemu amewaasa Mahakimu wa Mahakama za Mkoa wa Dodoma kuelewa na
kuzingatia Kanuni za Maadili za Maafisa wa Mahakama (Code of Conduct and Ethics
for Judicial Officers, 2020 (Government Notice 1001 of 2020) kwa kuwa ni
miongoni mwa miongozo muhimu katika kutekeleza majukumu yao.
Kiongozi huyo aliyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya
ndani yaliyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kuwaleta pamoja Mahakimu
wote wa Mahakama za Mkoa wa Dodoma. Mafunzo hayo yalifanyika mkoani humo jana tarehe
10 Juni, 2022 kwa lengo la kushirikishana, kubadilishana ujuzi, kukumbushana
majukumu na viwango bora vya utendaji kazi.
Sambamba na hilo, Mhe. Mdemu akamtaka Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kusimamia maadili ya Mahakimu katika vituo
vyote ndani ya Mkoa huo. Akisisitiza Jaji Mfawidhi huyo alisema, “Licha ya kuwa
tupo viongozi wengine tunaosimamia maadili ndani ya Kanda yote, ninakutaka Mhe.
Janeth Musaroche katika nafasi yako ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu
Mkazi Dodoma kusimamia maadili ya Mahakimu katika vituo vyote ndani ya Mkoa.”
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhe. Musaroche alitoa
wito kwa Mahakimu hao kuzingatia viapo vya kazi zao, kujiepusha na vitendo
viovu ikiwemo rushwa sambamba na kuzingatia maelekezo yanayotolewana viongozi
na yale yanayotolewa na Mahakama za juu kuhusu mamlaka waliyonayo katika
upokeaji na usikilizaji wa mashauri, utekelezaji wa hukumu pamoja na kuimarisha
mifumo ya masijala.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutaongeza kasi katika upokeaji, ufunguaji na
usikilizaji wa mashauri na kuyatolea uamuzi kwa wakati ili kuwezesha wananchi
kupata haki kwa wakati.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo mahsusi
yaliyotolewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha maadili katika utendaji kazi na
hatimaye kuboresha zaidi huduma za Mahakama zinazotolewa katika ngazi zote za
Mahakama nchini.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Janeth Musaroche akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mdemu mara baada ya kuhitimisha uwasilishaji wa mada katika mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni