Na Stephen Kapiga –Mwanza
Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mwanza leo tarehe 10 Juni, 2022 imefanya kikao cha kusukuma mashauri kwa kuwashirikisha
wadau mbalimbali ili kupanga mikakati ya pamoja yenye lengo la kuharakisha
utoaji wa haki kwa wananchi.
Wajumbe wa kikao hicho
kilichofanyika katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Buswelu-Mwanza
chini ya Mwenyekiti, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mhe. Monica Ndyekobora, walianza
kwa kujadili mashauri ya jinai yanayoendelea katika Mahakama zote za Mkoa wa
Mwanza ambapo ilibainika uwepo mdogo wa mlundikano.
Katika taarifa yake kwa
wajumbe hao, Mhe. Ndyekobora alibainisha kuwa mashauri ya jinai ambayo ni ya
mlundikano ni yale ambayo Mahakama haina mamlaka ya kuyasikiliza.
Hivyo amewapongeza Mahakimu
Wafawidhi wa Wilaya kwa kuondoa mashauri ya mlundikano katika vituo vyao. Alisema,
“Kipekee nawapongeza sana Wafawidhi wa Wilaya kwa kushirikia na ofisi ya mashtaka
katika Mkoa pamoja na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mwanza kwa kuwezesha
hili. Hii inaonesha ni jinsi gani tunavyozingatia agizo la Jaji Mkuu la
kuhakikisha mashauri yote ya jinai yanaisha ndani ya muda na hivyo kudhihirisha
haki inatendeka kwa wote na kwa wakati.”
Wajumbe waliohudhuria kikao
hicho ni Mwendesha Mashtaka Mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Afisa Uhamiaji wa Mkoa, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza, Mawakili wa Serikali, Mahakimu
Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zote za Mkoa pamoja na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa
wa Mwanza.
Katika kikao hicho, wajumbe
walifikia mikakati kadhaa ikiwemo kuhakikisha mashauri yote ya jinai yanasomwa maelezo
ya wali (PH) ndani ya siku saba tangu shauri kufunguliwa, kusikiliza ushahidi
kati ya siku saba na 14, huku utetezi ukitolewa kati ya siku ya 15 na 21 tangu kufunguliwa
kwa shauri husika.
Wajumbe hao pia waliweka msisitizo
wa kutoa uamuzi ndani ya siku 60 tangu kufunguliwa kwa shauri husika kwa
washitakiwa ambao wapo mahabusu, hatua ambayo itasaidia kuondoa msongamano gerezani.
Akizungumza katika kikao
hicho, Mwendesha Mashtaka Mkuu Mkoa wa Mwanza, Bi Bibiana Kileo aliwakumbusha wapelelezi
kuwaruhusu maaskari polisi wanaotakiwa kutoa ushahidi kufika mahakamani kwa
muda unaotakiwa na endapo itaonekana kuwa askari husika yupo mbali awezeshwe kutoa
ushahidi kwa njia ya “video conference”.
“Ndugu zangu wa ofisi ya
upelelezi kwa hili tunahitaji ushirikiano wa dhati, maana nyie ndio mnahusika
na ukamataji, hivyo ni rahisi kujua shahidi kutokana na yale mahojiano
mnayofanya. Kwa sasa hatuwezi kukwepa teknolojia, hivyo nawaomba tuondoke
kwenye yale mazoea ya zamani ya kuweka vikwazo kwa maaskari pale wanapohitaji
ruhusa ya kuja kutoa ushahidi,” alisema.
Kwa upande wake RCO aliwahakikishia
wajumbe wote kuwa ofisi yake itashirikiana vyema na ofisi ya mashtaka pamoja na
Mahakama kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati kwa wote.
“Upande wa ofisi ya
upelelezi kwa sasa nasi tunakimbia pamoja na teknolojia ikiwa pamoja na
kuwapatia mafunzo maafisa wetu, hivyo ni imani yangu kuwa tukiwa na mawasiliano
baina ya ofisi ya upelelezi na ofisi ya mashtaka hakuna shahidi atakayekwama
kufika mahakamani, cha msingi wito kwa mashahidi utolewe mapema na tuepuke
kuwashtukiza, kwani huenda wakawa wamepangiwa majukumu mengine kama wito
haukutolewa mapema,” alisema.
Naye mwakilishi wa
mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika aliahidi kuwakumbusha mawakili wote
kupanga ratiba zao vizuri ili kuepuka kuahirisha mashauri mara kwa mara
kutokana na ratiba zao kuingiliana na Mahakama za juu.
Kwa upande wa mashauri ya
madai, wajumbe hao walijiwekea mkakati wa kuyaendesha kwa mfumo wa vikao na pia
kutumia fomu ya maelezo ya shahidi pale inapohitajika kama sheria inavyoelekeza
ili kuokoa muda na kupunguza kuahirisha mara kwa mara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni