·Ni baada ya kuzabwa mabao 3-1 na Mahakama Sports Club
Na. Mwandishi wetu –Mahakama
Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Sports Club
Shinyanga jana tarehe 12 Juni, 2022 iligeuka kuwa kaa la moto baada ya
kuwasambaratisha Shinyanga Tanroad fc kwa ushindi wa mabao 3-1 kwenye mchezo wa
kirafiki uliofanyika katika viwanja vya Tanroad Shinyanga.
Kabumbu hiyo ambayo ilichezwa kuanzia majira ya saa 10.00 jioni ilianza
kwa kasi huku timu zote mbili zikionyesha kukamiana ambapo katika dakika za
mwanzo mwanzo kulikuwepo na kosa kosa za hapa na pale.
Hata hivyo, Mahakama Sports Club Shinyanga ilianza kuonyesha
makali yake katika dakika ya 35 ya mchezo mara baada ya Kiungo Punda Mshambuliaji
wake hatari Frank Obadia kupachika bao safi kufuatia pasi mpenyezo kutoka winga
ya kulia.
Hadi timu zote mbili zinaenda mapumziko (half
time) ilikuwa Mahakama Sports Club Shinyanga
iliyokuwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao Shinyanga Tanroad fc.
Mchezo katika kipindi cha pili pia ulianza kwa kasi
huku Mahakama Sports Club Shinyanga wakiendelea kulisakama lango la Shinyanga
Tanroad fc na katika dakika ya 50 wakafanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Nahodha
wao Benidicto Mtewa, ambaye ni beki wa pembeni.
Kufungwa kwa bao hilo kuliendeleza mashambulizi na
kama washambuliaji wa Mahakama Sports Club Shinyanga wangekuwa makini wangeweza
kupachika mabao mengi zaidi. Hata hivyo, katika dakika ya 66 Mshambuliaji
hatari Patrick Mluge akafanikiwa kupachika bao la tatu baada ya kupokea pasi
murua kutoka kwa kiungo maeneo ya katikati ya uwanja.
Shinyanga Tanroad fc wakazinduka majira ya jioni na
ilipofika dakika ya 86 ya mchezo wakafanikiwa kupata goli la kufutia machozi
kupitia mchezaji wao Mudrika Changulu baada ya wachezaji wa Mahakama Sports Club
Shinyanga kujiamini kupita kiasi kwa vile muda wa mchezo huo ulikuwa ukifikia
ukingoni.
Hadi mechi inamalizika kwa dakika zote 90, ubao wa
matangazo ulikuwa ukisomeka Mahakama Sports Club Shinyanga 3 huku Shinyanga
Tanroad fc 1.
Akizungumza kufuatia matokeao hayo, Mwenyekiti wa Timu
ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Wilson Dede amesema ushindi huo ni ishara nzuri ya maandalizi
kuelekea mashindano ya Shimiwi yanayotarajia kufanyika hivi karibuni. Amesema Mahakama
Sports imedhamiria kuchukua vikombe vingi zaidi kwenye mashindano hayo, ikiwemo
kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Kocha wa Mahakama Sports
Club Shinyanga na Mwenyekiti wa Michezo Shinyanga) Abdulmuumin Mbaraka (mwenye
tracksuit) akiwapongeza wachezaji wake baada ya kuibuka washindi kwa mabao 3-1
dhidi ya Shinyanga Tanroad fc 1.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni