Na Faustine Kapama – Mahakama
Meneja Mwendeshaji na Utawala (Governance
Practicing Manager) kutoka Benki ya Dunia, Bi Nicola Smithers ameipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa kutekeleza kwa ubora wa hali ya juu miradi mbalimbali
inayofadhiliwa na taasisi hiyo ya fedha hapa nchini.
Bi. Smithers ametoa pongezi hizo leo
tarehe 14 Juni, 2022 alipokutana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel ofisini kwake katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es
Salaam.
Kiongozi huyo Mwandamizi wa Benki ya
Dunia ameeleza kuridhika jinsi Mahakama ya Tanzania inavyotekeleza miradi hiyo na
kueleza jinsi inavyofanya vizuri
ukilinganisha na taasisi zingine. Ameahidi kuufahamisha ulimwengu kuja kujifunza
Tanzania.
Bi. Smithers ambaye aliambatana na
viongozi wengine kutoka Benki hiyo, Bw. Benjamin Mtesigwa na Bi Diana Mwaipopo
alibainisha kuwa kuna mambo mazuri alikuwa anayaona kwenye meza na hakuamini
kama Mahakama ya Tanzania ingeweza kufanya hivyo mara baada ya kufika nchini
kujionea utekelezaji wa miradi hiyo unavyofanyika.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania ameonyesha furaha yake ya kupokea ugeni huo ambao alikuwa
akiusubiri kwa muda mrefu. “Ni furaha yangu kuwaona hapa. Hatimaye June 14
imefika, karibuni sana mjisikie mko nyumbani,” aliwaambia wageni wake wakati
akiwakaribisha ofisini kwake.
Amemhakikishia kiongozi huyo kuwa Mahakama ya Tanzania
itaendeleza kutoa huduma za utoaji wa haki kwa wananchi kwa kasi, usahihi na
ufanisi zaidi kwa vile kauli mbiu yao ni kwamba kutofaulu sio na haitakuwa
chaguo lao.
Baada ya mazungumzo hayo mafupi,
ujumbe wa kiongozi huyo wa Benki ya Dunia ulielekea kwenye Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Temeke kinachojihusisha na mashauri ya Familia, Ndoa na Talaka
kujionea jinsi kinavyofanya kazi.
Akiwa katika Kituo hicho, Bi. Smithers
alipata nafasi ya kukutana na viongozi mbalimbali, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Kituo
hicho, Mhe. Ilvin Mgeta na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah
Sarawatt na baadaye kutembelea maeneo mbalimbali.
Kiongozi huyo alionyesha wazi
kushangazwa na uzuri wa Kituo hicho hasa baada ya kupitishwa kwenye vyumba
mbalimbali vya kusililizia mashauri na wadau mbalimbali wakiwemo Mawakili wa
Kujitegemea, Usitawi wa Jamii, Dawati la Jinsia na ilimchukua muda mrefu kuzungumza
na wadau alipofika kwenye chumba maalum wanachotumia wanawake kunyonyeshea
watoto.
Kadhalika, Bi. Smithers alitembelea
Mahakama Inayotembea ambayo kwa bahati nzuri ilikuwa katika maeneo hayo
ikisikiliza mashauri na kupata maelezo ya kina kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi
na Msimamizi wa Mahakama hiyo, Mhe. Moses Ndelwa wa namna inavyofanya kazi.
Katika maelezo yake, Mhe. Ndelwa amemweleza
kiongozi huyo kuwa Mahakama Inayotembea imebadilisha utoaji wa haki kwa
wananchi kwa kiasi kikubwa ambapo kwa sasa shauri linachukua chini ya siku 30 wakati
katika Mahakama za kawaida shauri hilo hilo linachukua miezi sita.
Akizunguza baada ya ziara hiyo, Mkuu
wa Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amesema
kuwa ujio wa kiongozi huyo ni nafasi nzuri kwa vile Mahakama ya Tanzania inajiandaa
kwenye mradi unaofuata ambao utahusisha upanuzi mkubwa wa huduma za kimahakama
kwenye mikoa yote Tanzania Bara ambayo haina Mahakama Kuu.
“Tunatarajia kujenga Vituo Jumuishi vingine katika mikoa hiyo. Katika mradi unaoisha tumejenga Vituo sita na mradi unaokuja tunajenga vingine tisa na ikiwezekana 12 kutegemea na uwepo wa fedha, lakini pia kutakuwepo na nyongeza ya Mahakama zinazotembea sita kwenda mikoa mbalimbali,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Meneja Mwendeshaji na Utawala (Governance Practicing Manager) kutoka Benki ya Dunia, Bi Nicola Smithers (hayupo katika picha) wakati Meneja huyo alipomtembelea Mtendaji Mkuu ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
Meneja Mwendeshaji na Utawala (Governance Practicing Manager) kutoka Benki ya Dunia, Bi Nicola Smithers (wa pili kushoto). Pamoja nao ni Maafisa walioambatana na Meneja huyo kutoka Benki ya Dunia.
Meneja Mwendeshaji na Utawala (Governance Practicing Manager) kutoka Benki ya Dunia, Bi Nicola Smithers (wa tatu kushoto). Pamoja nao ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (wa kwanza kulia), wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, wa pili kushoto ni Bw. Benjamin Mtesigwa, Afisa Kutoka Benki ya Dunia aliyeambatana na Bi. Nicola na wa pili kulia ni Bi. Diana Mwaipopo kutoka Benki ya Dunia.
Meneja Mwendeshaji na Utawala (Governance Practicing Manager) kutoka Benki ya Dunia, Bi Nicola Smithers (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa kutoka Mahakama wakati alipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Temeke. Wa pili kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, wa tatu kushoto ni Naibu Msajili wa Kituo hicho, Mhe. Mary Moyo na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha.
Meneja Mwendeshaji na Utawala (Governance Practicing Manager) kutoka Benki ya Dunia, Bi Nicola Smithers ( wa pili kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mratibu wa Mahakama inayotembea (Mobile Court), Mhe. Moses Ndelwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni