Na Ibrahim Mdachi – IJA Lushoto
Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewataka
Mahakimu kuzingatia mwongozo wa adhabu na kujiepuka kujihusisha na vitendo vya
rushwa ili kujenga jamii inayojali haki kwa kila mmoja na kuwafanya wananchi
waendelee kuwa na imani na Mahakama.
Mhe. Chuma ametoa wito
huo jana tarehe 13 Juni, 2022 mjini hapa alipokuwa akifungua mafunzo ya siku
tatu yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kilichopo mkoani Tanga ambayo
yamewaleta pamoja Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na
utekezaji wa amri za Mahakama.
Mafunzo hayo
yanayoratibiwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo hicho kupitia
ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania zinazohusika
na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) yanalenga kuwajengea uwezo Mahakimu
hao kutekeza jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Chuma amebainisha
kuwa Mahakimu wanaopokea rushwa wanaharibu sifa ya Mahakama kwa umma, ikiwemo
kujenga sifa mbaya kwa wananchi, hivyo akawasisitiza kutoa hukumu kwa kufuata
mwangozo uliuopo.
Alitanabaisha pia kuwa
kimsingi mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa mwongozo wa
utoaji adhabu ambao ni miongoni mwa nyenzo za maafisa wa Mahakama katika
mchakato wa utoaji wa adhabu kuwa halali na usiotiliwa shaka na wadaawa
wanaohusika katika mashauri mahakamani wakiwemo washtakiwa, waathiriwa,
wapelelezi, mawakili wa utetezi, waendesha mashtaka na umma kwa ujumla.
Mhe. Chuma alisema kuwa
ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kupitia mafunzo hayo uelewa wa mwongozo wa
utoaji adhabu utaongezeka, hivyo kutumika ipasavyo katika mashauri hasa ya
rushwa, uzoefu utakaopatikana utafikishwa kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao
hawakufanikiwa kupata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Akitoa maelezo mafupi
kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya
BSAAT ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha alisema kuwa, program hiyo inayofadhiliwa
na Serikali ya Uingereza kwa kushirikana na Umoja Ulaya (EU) na kuratibiwa na
Ofisi ya Rais, Ikulu ilianza kutekelezwa mwaka 2018/2019 ikijumuisha taasisi tisa
nufaika ambazo ni wadau katika mnyororo wa haki jinai ikiwemo Mahakama kama
mdau muhimu katika utiaji wa haki.
Bw. Magoha aliongeza
kuwa program hiyo imelenga kupunguza vitendo vya rushwa kama kikwazo cha
kupunguza kiwango cha umasikini kwa Watanzania, kuboresha uadilifu, kuboresha
uwezo na uratibu wa mfumo wa haki jinai katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa
na kuongeza imani kwa umma juu ya utendaji kazi wa Mahakama.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkuu wa Chuo Bw. Goodluck Chuwa alisema kuwa, ni takribana miaka mitano tangu
chuo kimeamua kujikita katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuundwa kwake
kitahakikisha kuwa kinaendelea kuyaratibu mafunzo mbalimbali kwa weledi mkubwa
kwa lengo la kuleta tija kwa Mahakama na wadau wengine wa sheria nchini.
Ufunguzi wa mafunzo
hayo ulihudhuliwa na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya Lushoto, Mhe. Rose Ngoka, Naibu
Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Fatihiya Massawe, sambamba na
wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania akiwemo Naibu Msajili, Mhe. Victoria
Nongwa, Mhe. Naibu Msajili Wanja Hamza na Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Richard
Kabate.
Mafunzo haya ni
mwendelezo wa jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kuwajengea uwezo maafisa
wa Mahakama wanapotekeleza majukumu yao sambamab na jitihada katika kusukuma gurudumu la utoaji wa haki
kwa wakati kwa wananchi.
Kaimu Mkuu wa Chuo,
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Mratibu wa Programu ya BSAAT, Mahakama ya Tanzania Bw. Stephen Magoha akisongea kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.
Picha ya kumbukumbu ya meza kuu na wawezeshaji kutoka Mahakama ya Tanzania (waliosimama), Mhe Victoria Nongwa, Naibu Msajili, (katikati) Mhe Richard Kabate, Hakimu Mkazi Mkuu (kulia) na Mhe Wanja Hamza, Naibu Msajili (kushoto).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni