Na Faustine Kapama – Mahakama.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, jana tarehe 14 Juni, 2022 alitembelea
Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo kushuhudia shughuli mbalimbali za kimahakama na
kutoa maagizo 12 yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kuharakisha utoaji wa haki kwa
wananchi.
Mhe.
Chuma alipata pia nafasi ya kuongea na watumishi wa Mahakama hiyo na kubaini
changamoto mbalimbali, ikiwemo mlundikano wa mashauri na kuagiza uwekwe mkakati
wa kuuondosha haraka.
Katika
mazungumzo yake, Msajili Mkuu pia alihimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) katika kusajili na kusikiliza mashauri. Kadhalika,
alielekeza watumishi kuendelea kuhuisha taarifa za mashauri kwenye mfumo wa
JSDS2.
Amewahimiza
Mahakimu kufikisha idadi ya mashauri 250 kwa mwaka ambayoyanaelekezwa na
viongozi wa Mahakama. Sambamba na hilo, Msajili Mkuu aliwahimiza Mahakimu
kuendelea kutoa nakala za hukumu na mwenendo wa mashauri kwa wakati.
Aidha, Mhe.
Chuma aliwataka viongozi wa Mahakama hiyo kuendelea kuwa wabunifu katika
kutatua changamoto mbalimbali za watumishi na zile ambazo hawana uwezo nazo kuziwasilisha
katika mamlaka husika.
Msajili
Mkuu pia alisisitiza maadili ya kazi,
kutekeleza maelekezo ya viongozi wa Mahakama, watumishi kufanya kazi kwa
bidii na kuendelea kupendana, kufanya kazi kwa pamoja (team work) na kusaidiana
katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kwa
upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Bagamoyo Mhe. Sameera
Suleman alimshukuru Msajili Mkuu kwa ujio wake. Alimjulisha kuwa wamejiwekea
mkakati wa kumaliza mashauri ya mlundikano ifikapo tarehe 31 Julai, 2022 na kuahidi
kuzingatia yote aliyowaelekeza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni