Alhamisi, 16 Juni 2022

TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YAFANYA USAILI KIELEKITRONIKI KWA MARA YA KWANZA

 Na Lydia Churi-Dar es Salaam

Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mara ya kwanza imefanya usaili kwa njia ya Kielekitroniki kwa kutumia akili bandia (Artificial Intelligence) katika mchakato wa ajira za watumishi 207 wa kada mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa usaili wa hatua ya kwanza jijini Dar es salaam, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema jumla ya Wasailiwa 573 ambao ni sawa na asilimia 80.36 ya Wasailiwa 713 waliochaguliwa kufanya usaili awamu ya kwanza walihudhuria na kufanya usaili huo kwa njia ya kielekitroniki.

Alisema Tume iliandaa vituo sita katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya usaili huo ili kurahisisha mchakato huo na kupunguza gharama. Vituo hivyo vipo Dar es salaam, kilichokuwa na wasailiwa 296, Mwanza 89, Mbeya 52, Dodoma 46, Morogoro 32 na Arusha kilichokuwa na wasailiwa 58.

Akielezea namna usaili huo ulivyofanyika, Katibu wa Tume hiyo alisema kila msailiwa alipewa maswali kwa njia ya mfumo wa kielekitroniki na alipomaliza, maswali hayo yalisasahihishwa na mfumo huo hatua iliyomwezesha msailiwa kutoka katika chumba cha usaili akiwa tayari anajua matokeo yake.

Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel, usaili kwa kutumia mfumo wa kielekitroniki umesaidia kwa kiasi kikubwa kuipunguzia gharama Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na wasailiwa ambao baadhi yao wangelazimika kusafiri umbali mrefu kufika jijini Dar es salaam kwa ajili ya kufanya usaili.

“Matumizi ya mfumo wa kielekitroniki pia yamesaidia kurahisisha mchakato mzima wa ajira na kuokoa muda ambao ungetumika katika kusahihisha na kupanga matokeo. Unaleta uwazi na kuondoa suala la watu kufahamiana na kusaidiana”, alisema.

 Naye mmoja wa wasailiwa wa kada ya Hakimu Mkazi ll, Bw. Hussein Hamidu Ramadhani akizungumzia usaili huo alisema ameufurahia kwa kuwa unaendana na mabadiliko ya Teknolojia duniani ambapo alisema Hakimu wa kizazi kipya hana budi kufahamu Tehama ili aendane na wakati.

Juni 3. 2022, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilitangaza nafasi 207 za ajira kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika kada za Hakimu Mkazi ll (20), Afisa Utumishi ll (4), Afisa Tawala ll (5), Afisa Hesabu ll (6), Afisa Ukaguzi wa Ndani (8), Msaidizi wa Hesabu (11), Msaidizi wa Kumbukumbu ll (38), Katibu Mahsusi ll (80) na Dereva ll ( 35).

Sehemu ya Wasailiwa wa nafasi 207 za ajira ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania zilizotangazwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kada mbalimbali wakiwa kwenye Usaili awamu ya kwanza uliofanyika jana jijini Dar es salaam pamoja na mikoa ya Mwanza, Dodoma, Morogoro, Arusha na Mbeya. Kwa mara ya kwanza Tume imefanya usaili kwa njia ya Kielekitroniki kwa kutumia akili bandia (Artificial Intelligence).

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza mara baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya Usaili jijini Dar es salaam. 

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akimwelezea jambo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Bi. Beatrice Patrick kabla ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya Usaili jana jijini Dar es salaam. 
Sehemu ya Wasailiwa wa nafasi 207 za ajira ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania zilizotangazwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kada mbalimbali wakiwa kwenye Usaili awamu ya kwanza uliofanyika jana jijini Dar es salaam pamoja na baadhi ya maeneo mengine nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni