Na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma.
Jaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Adam Mambi amewahimiza Wahasibu na
Wakaguzi wa Ndani wa Mahakama ya Tanzania kusoma, kuelewa na kuitumia Sheria ya
Miamala ya Kielektroniki “Electronic Transaction Act” ya mwaka 2015 pamoja na
Sheria ya Serikali Mtandao “e–Government Act” ya mwaka 2019 ili kuongeza weledi
na ufanisi, kwani kwa kuzitafsiri vizuri itaongeza tija katika kutekeleza
majukumu yao ya kila siku.
Akifanya mapitio ya tafsiri
na matumizi ya Sheria hizo katika mafunzo ya Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani
yanayofanyika katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma
hivi karibuni kama Mwezeshaji, Jaji Mambi alisema kuwa sheria hizo zinalenga utekelezaji
wa Mpango Mkakati wa Mahakama kwenye nguzo zote za utawala, uwajibikaji na
usimamizi wa rasilimali; haki kufikika na kupatikana kwa wakati na kuimarisha
imani kwa umma na ushirikishwaji wa wadau.
“Malengo ya uwepo wa Sheria
ya Miamala ya Kielektroniki ni kujielekeza katika kuweka utambuzi wa kisheria
wa miamala ya kielektroniki, huduma za Serikali mtandao, matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ukusanyaji wa ushahidi, kukubalika kwa
ushahidi wa kielektroniki, urahisishaji wa matumizi ya sahihi salama za
kielektroniki na mambo mengine mtambuka yanayohusiana na hayo”, Dkt. Mambi
alisema.
Akifafanua sheria hiyo, Jaji
Mambi alisema Sheria ya Miamala ya Kielektroniki namba 13 ya mwaka 2015
inaelekeza masuala mbalimbali ikiwemo malipo ya fedha kielekroniki, usimamizi
wa fedha na pia utekelezaji wa sheria ya miamala ya kielektroniki. Amesema
katika Sheria tajwa vifungu vya 13 na 15 ni muhimu katika utekelezaji wa
majukumu ya kiuhasibu hasa kwenye kufanya malipo kimtandao.
“Kifungu cha 13 cha sheria ya
miamala ya kielektroniki namba 13 ya mwaka 2015 kinazungumzia zaidi serikali
mtandao, kinatambua matumizi ya serikali mtandao ama huduma za serikali
mtandaoni (E-Government). Kifungu cha 15 cha sheria hiyo kinaelezea malipo na
uwasilishaji wa stakabadhi kielektroniki na hayo mambo ni ya msingi katika
utekelezaji wa shughuli za kihasibu, aliongeza Dkt. Mambi.
Kwa upande wa uhalali wa
muamala wa kielektroniki, Jaji Mambi alisema, Kifungu cha 5, kifungu
kidogo cha kwanza (1) kinaelekeza endapo sheria inahitaji taarifa au muamala
kuwa katika namna iliyoainishwa isiyo ya kielektroniki au kimaandishi, masharti
hayo yatakuwa yametimizwa na taarifa au muamala wa kielektroniki ambayo imewekwa
katika namna sawa au inayokaribiana na namna maalum isiyo ya kielektroniki, inaweza
kufikiwa na mtu mwingine kwa ajili ya rejea, ina uwezo wa kuhifadhiwa na mtu
huyo mwingine. Alisema pia kuwa kifungu cha 5(2) na Kifungu kidogo cha pili (2)
kitatumika iwapo katika maandishi ni ya lazima au iwapo sheria inaainisha
madhara ya taarifa ambayo haiko kimaandishi.
Aidha, Dkt. Mambi alieleza
kuwa, malipo ya fedha na utoaji wa stakabadhi kwa njia ya kielektroniki
yameainishwa katika Kifungu cha 15 cha sheria hiyo kuwa, endapo sheria
inahitaji malipo kufanyika, masharti hayo yatakuwa yametekelezwa iwapo malipo
yatakuwa yamefanyika kwa njia ya kielektroniki na kukidhi masharti yoyote
yaliyotolewa na sheria nyingine husika.
Kwa mujibu wa
sheria hiyo, utoaji wa stakabadhi yoyote ya malipo, masharti hayo yatakuwa
yametekelezwa iwapo stakabadhi hiyo itakuwa katika mfumo wa ujumbe wa
kielektroniki na ujumbe kusomeka na unaeleweka kiasi kwamba unaweza kutumika
katika rejea.
Washiriki wa mafunzo hayo ya
Waasibu na Wakaguzi wa Ndani wakaombwa kutosita kutoa elimu waliyoipata kwa
watumishi wengine ambao hawakupata nafasi hiyo adhimu ya kushiriki ili
kuwajengea uwezo na uelewa wa pamoja katika kusukuma gurudumu la shughuli za taasisi.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama.)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni