Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama
Mahakama Kuu ya Tanzania (Masijala Kuu) Dar es
Salaam imempa kibali aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Bw. Ezekiah Oluoch, kupinga uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye amethibitisha adhabu ya kufukuzwa kazi kwenye utumishi wa umma.
Jaji Sekela Moshi amefikia uamuzi huo baada ya kuyakubali
maombi, ambayo maelezo na mawasilisho yake hayakupingwa mahakamani, yaliyowasilishwa
na Mwalimu Oluoch, mwombaji, dhidi ya wajibu maombi wawili, Katibu Mkuu
Kiongozi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“(….) nimeona kuwa maelezo yake (mwombaji) yanajitosheleza
kumpa kibali cha kufungua shauri la msingi la mapitio ya Mahakama (judicial
review) kwani kuna shauri la msingi kuhusu utaratibu uliotumika kumwachisha
kazi, pia ana maslahi kwa kuwa yeye ndiye aliyeachishwa kazi,”amesema.
Aidha, Mhe. Moshi amebainisha kuwa maombi hayo ya
kibali yamaletwa ndani ya muda kwa mujibu wa Kanuni ya 6 ya sheria ya Law
Reform Fatal Accident Provisions Miscellaneous Provision (Judicial Review
Procedure & Fees) 2014 ambayo ni ndani ya miezi sita.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Moshi alisema kuwa
mwombaji anatakiwa athibitishe mbele ya
Mahakama hiyo mambo makuu matatu ya kisheria kabla ya kupewa kibali cha
kufungua shauri la mapitio ya Mahakama.
“Kwanza kabisa anatakiwa aonyeshe kuwa kuna kesi ya
msingi, pili anatakiwa kuonyesha kuwa shauri lakelimefunguiiwa ndani ya miezi
sita na miezi hiyo inaanza kuhesabika tangu chanzo cha mgogoro ulivyoanza, na
tatu anatakiwa aonyeshe kuwa ana maslahi muhimu katika maombi ya msingi,”
alisema.
Baada ya kuangalia aya ya 51, 52,
41,44,45,42,46,47,3,35,39,21, na 23 ya maelezo ya mwombaji na mawasilisho yake
hayakupingwa hapa mahakamani, Jaji huyo aliona kuwa maelezo hayo yanajitosheleza
kumpa kibali cha kufungua shauri la msingi la mapitio ya Mahakama.
“Kwa hiyo, maombi haya yamekubaliwa baada ya
kuzinqatia mambo yote yaliyojadiliwa katika uamuzi huu. Inaamriwa hivyo,” Jaji
Moshi amesema.
Mwombaji aliajiriwa kwenye utumishi wa umma tangu
tarehe 01 Julai, 1993 na mwajiri wake alikuwa ni Katibu Mkuu wa iliyokuwa
Wizara ya Elimu na Utamaduni ambayo kwa sasa ni Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia.
Tangu awe mtumishi wa umma, hakuwahi kujulishwa kuwa
mwajiri wake alibadilika na kuwa ni Manispaa ya Ilala kwa sasa ni Jiji la Dar
es Salaam. Mwombaji akiwa ni mtumishi wa umma, alijiunga na Chama cha Walimu
Tanzania (CWT) ambacho ni Chama cha Wafanyakazi.
Akiwa kama
mwanachama wa CWT, aligombea na kuchaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CWT kwa
muda wa vipindi vinne mfululizo kuanzia Mei, 2000 (2000-2005), Mei
2005(2005-2010), Mei 2010(2010-2015) na Mei 2015(2015-2020).
Tarehe 20 Februari, 2017, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma alimwandikia barua ya kumtaka aidha aache
nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu wa CWT ili arudi kwenye utumishi wa umma au
aajiriwe na CWT.
Katiba ya CWT hairuhusu kiongozi wa kuchaguliwa
kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu kuajiriwa na CWT katika masharti ya kudumu.
Kwa kuwa yote yalikuwa hayatekelezeki, mwombaji hakufanya uchaguzi wowote ule.
Matokeo yake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti
ya Utumishi wa Umma alimwandikia barua ya kumwondoa kazini tarehe 16 Machi,
2017 bila kuwa na mamlaka.
Mwombaji hakuridhika na uamuzi huo na alifungua shauri
katika Mahakama Kuu kuomba kibali na baada ya kibali kutolewa, alifungua shauri
la mapitio ya Mahakama kupinga kuondolewa kwenye utumishi wa umma.
Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali na
Mahakama. Kwa kuwa hakuridhika na uamuzi
huo, mwombaji alikata rufaa Mahakama ya Rufaa.
Tarehe 06 Januari, 2020 Mahakama ya Rufani ya
Tanzania ilifuta mchakato wote uliomwondoa mwombaji kwenye utumishi wa umma kwa
sababu alihukumiwa bila ya kusikilizwa na aliyefanya uamuzi ya kumwondoa hakuwa
na mamlaka.
Baada ya Mahakama ya Rufani kufuta mchakato huo,
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma hakuridhika na uamuzi
ya Mahakama ya Rufani, hivyo alianzisha upya mchakato wa kumfukuza kazi mwombaji
kwenye utumishi wa umma.
Kwa kuanzishwa upya kwa mchakato huo, mwombaji alifukuzwa
tena kazi na Kamati ya Nidhamu ya Tume ya Utumishi wa Walimu ya Manispaa ya Ilala
tarehe 22 Mei, 2020.
Mwombaji hakuridhika na kufukuzwa kwake kazi na
alikata rufaa kwenye Tume ya Utumishi wa Walimu kama sheria inavyoelekeza
lakini rufaa yake ilitupiliwa mbali.
Kufuatia uamuzi huo wa Tume, mwombaji alikata rufaa
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Mamlaka ya mwisho ya Rufaa.
Tarehe 06 Januari, 2022, Katibu Mkuu Kiongozi
alimjulisha mwombaji kwa barua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ametupilia mbali rufaa yake na ameridhia adhabu ya kufukuzwa kazi kwenye
utumishi wa umma.
Mwombaji, kwa mara nyingine tena, hakuridhika na aliamua
kuwasilisha maombi katika Mahakama Kuu ili kupata kibali cha kumwezesha
kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kupinga uamuzi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni