Jumanne, 19 Julai 2022

MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA ATAKA UPENDO, HAKI KUTAWALA

 Na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wibert Chuma amewataka Mahakimu Wakazi wapya kutekeleza majukumu yao kwenye vituo watakavyopangiwa kwa upendo na haki.

Mhe. Chuma ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Julai, 2022 mjini hapa wakati wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu ambayo yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Amesema wapo Mahakimu watapangiwa vituo vya kazi ambavyo sio vya asili yao au ya wazazi wao, hivyo pindi watakapofika sehemu hizo watoe huduma kama vile ambavyo wangetoa wangekuwa kwao.

“Lazima muelewe kwamba mtakwenda kufanya kazi pengine katika maeneo ambayo sio mlipozaliwa au wazazi wenu wanaishi…nendeni mkatoe huduma kwa kuzingatia upendo na haki kama ambavyo mgependa Mahakimu wenzenu watoe haki na upendo katika eneo la kwenu” amesisitiza.

Aidha Msajili Mkuu huyo wa Mahakama amewataka watumishi hao kuwajali wateja wa ndani na nje wanapokuwa wanatoa huduma za haki na kuwasilikiza wale wanaohitaji ushauri.

Mhe. Chuma amewasisitiza wawe wanaonyesha huduma zenye upendo kwa  wateja wanapoingia katika ofisi zao kwa kuwajali ili waendelea kuitangaza Mahakama ya Tanzania vizuri ndani na nje.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Beatrice Patrick amewataka watumishi wapya kuwa waatifu kwa Serikali iliyopo madarakani.

Amesema watumishi wa Mahakama hawapaswi kushiriki katika makundi ya mitandao ya kijamii kwa kutoa maoni ambayo yanaidhalilisha taswira ya Serikali mbele ya jamii.

Aidha, Bibi Beatrice amewakumbusha kutumia muda wa mwajiri wao kwa uaminifu katika kuwahuduma wananchi ili waweze kupata haki wanazitajajia kutoka mahakamani.

Amesema kuwa ni makosa kwa watumishi wa umma kutumia rasilimali za Serikali, ikiwemo magari na muda wa kuwa ofisini kwa maslahi binafsi.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wibert Chuma akijibu maswali mbalimbali mbele ya Mahakimu Wakazi na Wasaidizi wa Kumbukumbu wakati wa mafunzo elekezi yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bibi Beatrice Patrick akitoa mada kuhusu haki na wajibu  wakati wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu ambayo yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Mahakama ya Tanzania Sebastian Lacha akitoa mada kuhusu Utekelezaji wa Mapango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania katika mafunzo elekezi ya Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu ambayo yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi na Wasaidizi wa Kumbukumbu (juu na chini) wakifuatilia mafunzo elekezi yanayoendelea katika chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni