Jumanne, 19 Julai 2022

NEEMA KUFUNULIWA KWA MAHAKIMU MAHAKAMA ZA MWANZO

 Na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto

Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wanatarajiwa kupewa Kompyuta mpakato na Vishikwambi (tablets) ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kuwa na mazingira mazuri ya kuendesha mashauri bila kukwama.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 19 Julai, 2022 mjini hapa na Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha wakati akitoa mada kwenye mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Mada hiyo ilihusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Uboreshaji wa Mahakama wa 2020/21 hadi 2024/25. Amesema kuwa hatua hiyo itawawezesha Mahakimu hao kusikiliza mashauri hata mtuhumiwa amekosa gari la kumpeleka mahakamani kutoka Mahabusu kwa sababu ya kukosekana kwa usafiri.

Mhe. Dkt. Rumisha amesema hali hiyo itasaidia pia kuhakikisha mashauri yanaendelea kusikilizwa, hivyo kuepusha kuahirishwa na kusababisha uwepo wa mrundikano katika baadhi ya Mahakama.

Ameongeza kuwa kutakuwepo na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo wahusika watapewa muda wa mawasiliano(bando)  kwa mwaka mzima ili Mahakimu hao aweze kufanya kazi vizuri bila vikwazo, hivyo kuwafanya hawakwami wakati wanapotumia Vishikwambi hivyo.

Mhe. Dkt. Rumisha amesema lengo la Mahakama ni kuhakikisha kuwa mashauri yanasikilizwa kwa wakati, kwa haki na katika mazingira sawa kwa wote.

Katika hatua nyingine, Mahakama kupitia Kitengo cha Uboreshaji inatarajia kuongeza Mahakama zinazotembea sita ili kusogeza huduma za utoaji haki kwa wananchi wa maeneo ambayo hayana huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Rumisha, matumizi ya Mahakama hizo katika Awamu ya Kwanza katika Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza yameonyesha mafanikio makubwa kwa kusikiliza mashauri mengi na kutoa uamuzi katika maeneo ambayo hayana huduma za kimahakama kwa kutumia majengo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama amesema Mahakama iko katika hatua ya mwisho kuwezesha mfumo wa kutafsiri na kuchapisha uamuzi wa mashauri ya Mahakimu na Majaji kuanza kufanya kazi  nchini Tanzania.

Amesema mfumo huo ambao unatarajia kuanza ndani ya mwaka huu utamwezesha mhusika kupata nakala kwa lugha anayoielewa pale Hakimu au Jaji anapomaliza kusoma hukumu.

Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akitoa mada kuhusu Mpango wa Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano wakati wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Mahakama ya Tanzania Sebastian Lacha akitoa mada kuhusu Utekelezaji wa Mapango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania katika mafunzo elekezi ya Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu ambayo yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi na Wasaidizi wa Kumbukumbu (juu na chini) wakifuatilia mafunzo elekezi yanayoendelea katika chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto).


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni