Na Magreth Kinabo - Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameviasa vyuo vya elimu ya
sheria nchini vibadili mitaala yao ili kuwawezesha wahitimu wa taaluma hiyo kutoa
huduma ya sheria kulingana na karne ya 21 ya teknolojia.
Akizungumza
katika sherehe ya 66 ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya 335`
iliyofanyika Juni 8, mwaka huu katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es
Salaam, Prof. Juma amesema hivi sasa hali ya nchi na dunia imebadilika, hivyo
hata wao katika taaluma hiyo wanahitaji mabadiliko.
“Tuwe
na mitaala ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo vikuu vya sheria kuweza kuishi na
kufanya kazi katika dunia ya teknolojia. Vyuo vikuu lazima vitoe elimu hiyo ili
kuwawezesha wanasheria kufanya kazi katika karne 21 ya teknolojia,” alisema Prof.Juma.
Aliongeza
kwamba Shule ya Sheria kwa Vitendo; na Skuli ya Sheria Zanzibar vinawajibu wa
kuwatayarisha wahitimu wa Sheria Tanzania kuweza kutoa huduma zinazolingana na
mahitaji ya karne ya 21.
Alisema
wahitimu hao, wajitayarisheni kufanya kazi za kiuwakili pamoja na kazi zisizo
za kiuwakili. Kazi za kushirikiana na wanataaluma wa fani nyingine ndani na nje
ya Tanzania.
Hivyo
wanapaswa kuwa tayari wa kukubali ajira za muda mfupi mfupi, katika sekta
binafsi na kwa malipo chini ya matarajio yao kwa kuwa zama za Sekta ya Umma
kama injini pekee ya kuendesha shughuli za kisiasa, kiuchumi, biashara na
uwekezaji Tanzania zimepitwa na wakati.
“Katika
hizi zama za utandawazi, ushindani na matumizi makubwa ya teknolojia; Mawakili
lazima kujiongezea maarifa mapya na kubadilika kifikra na kimtazamo ili muweze
kukidhi ushindani wa uchumi wa sasa wa Tanzania na dunia unaotegemea sekta
binafsi,’’ alisisitiza.
Alisema
ajira ya mawakili katika sekta binafsi, sekta ya biashara na Sekta ya uwekezaji
inapunguza utatuzi wa migogoro kwa taratibu za kimahakama ambazo zimelaumiwa
kwa ucheleweshwaji na matumizi ya mapingamizi na kuegemea taratibu za kiufundi
katika utoaji wa haki.
“Mawakili
jitayarisheni kufanya kazi za Waendesha Maridhiano, Majadiliano, Upatanishi na
Usuluhishi (Reconciliation, Negotiation, Mediation and Arbitration). Tanzania
imegundua kuwa ucheleweshwaji wa mashauri ambao huchangiwa na matumizi ya kesi
za mahakama, hazikidhi mahitaji ya mazingira bora usuluhishi kwa faida ya
biashara na uwekezaji wa ndani na wa kutoka nje ya Tanzania,” alisema huku
akiongeza kwamba ni eneo linahitaji kuimarishwa.
Alisema
Mahakama ya Tanzania imewekeza katika mifumo ya teknolojia na akili bandia kupitia
Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA)-Lushoto, Hivyo imejipanga kuwafundisha
watumishi wote wapate ujuzi wa masuala ya kidigitali ikiwa ni hatua ya kuendana
na karne ya 21 kwa hali mali.
Alifafanua
kuwa Mahakama tayari imeanza kuwajengea uwezo wa kubadili fikra ya kufanya kazi
katika Tanzania na Dunia ya Kidigitali.
‘‘Nyie
mnaohitimu leo ni mashahidi, usaili wenu na kujisajili kwenu kuwa Mawakili
mmetumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia mifumo mbalimbali
tuliyonayo mahakamani,yuko mmoja kati yenu nimemsaili akiwa India na nimeambiwa
leo tuko naye hapa ameisharudi,”alisema.
Alisema huo ni mwanzo kwa wale mtakaokuja
kufanya kazi mahakamani, basi tambueni kesi zote kuanzia kusajili, kusikiliza
mpaka upatikanaji wa maamuzi yote ni kwa njia ya TEHAMA. Matumizi ya TEHAMA ni
nyenzo muhimu kwa Mahakama katika utoaji haki na kuharakisha usikilizwaji wa
mashauri.
Kwa
upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa ambaye
amemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliwataka mawakili hao,kutoa
huduma ya utoaji haki iliyobora kwa kuzingatia maadili, sheria, kanuni na
taratibu.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Prof. Edward Hosea, aliwataka kutoa msaada wa elimu ya kisheria kwa Watanzania kwa kuwa wajibu na jukumu lao ni kutoa haki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni