Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Ujumbe wa Benki ya Dunia umeipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu inayotumika
katika utoaji wa haki katika maeneo mbalimbali nchini.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni mjini Arusha
na Kiongozi wa Ujumbe kutoka Benki hiyo, Bi. Christine Owuor katika kikao cha
majumuisho ya ziara ya wiki mbili kukagua utekezaji wa awamu ya kwanza na
maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama
nchini awamu ya pili.
Kiongozi huyo alisema miradi iliyotekelezwa katika
awamu ya kwanza imesaidia kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi
katika maeneo yao.
“Tumetembelea miradi katika maeneo mbalimbali hapa
nchini Tanzania …tumefurahishwa na utekelezaji wake kwa kuwa miradi mingine
imesaidia kusogeza karibu huduma za upatikajini wa haki kwa wanyonge wakiwemo
wanawake,” amesema.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliuhakikishia Ujumbe huo kuwa
katika awamu ya pili watahakikisha wanatumia fedha za mkopo zilizotengwa kupeleka
huduma ya upatikanaji haki hasa kwa wananchi walio mbali kama walivyofanya wakati
wa utekelezaji wa awamu ya kwanza.
Alisema hakuna fedha yoyote itakayotumika kinyume
cha matumizi iliyopangiwa ambapo lengo la Mahakama ni kuhakikisha kuwa fedha
hiyo inasaidia kuongeza idadi ya huduma za kimahakama kuanzia Mahakama za
Mwanzo hadi Mahakama Kuu.
Prof. Ole Gabriel alisema katika awamu ya kwanza
walipata mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 65, sawa na bilioni 160 za
Kitanzania ambazo zimesaidia kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita katika
Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza , Dodoma na Arusha na Mahakama za Wilaya na zile za Mwanzo
katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Alibainishsha pia kuwa katika awamu ya pili wamepata
mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 90, sawa na bilioni
200 za Kitanzania ambazo watazitumia kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki zaidi
na Mahakama za chini katika maeneo ambayo bado hayana huduma hizo za kimahakama.
Prof. Ole Gabriel alisema lengo la Mahakama ya
Tanzania ni kuhakikisha mwananchi anapata huduma ya upatikanaji wa haki katika
maeneo ya karibu na anatumia muda mfupi ili sehemu iliyobaki aitumie katika
uzalishaji wa mali.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Ujumbe wa Benki ya Dunia na watumishi wa Mahakama ya Tanzania hivi karibuni mjini Arusha mara baada ya ziara ya wiki mbili kutembelea miradi inayotekelezwa na Mahakama kwa mkopo nafuu wa Benki hiyo.
Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor akieleza jambo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya wiki mbili ya kukagua utekezaji wa awamu ya kwanza na maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama nchini awamu ya pili.
Sehemu ya wakuu wa Idara, Vitengo na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania (juu na chini) wakiwa katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Ujumbe wa Benki ya Dunia kukagua utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama nchini Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni