Jumatatu, 18 Julai 2022

MAHAKAMA MKOANI MOROGORO KUZIPA KIPAUMBELE KESI ZA UJANGIRI

 Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Makakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amesema kuwa Mahakama Kanda ya Morogoro itahakikisha kesi zote zinazogusa Hifadhi za Taifa zinapewa kipaumbele kukabiliana na ujangiri.

Mhe. Ngwembe alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akichangia taarifa fupi iliyosomwa kwake na Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi, Kamishna Msaidizi Mathew Mombo, ambaye alitaja ujangiri kuwa miongoni mwa changamoto katika hifadhi hiyo. Jaji Mfawidhi huyo alihimiza wanaohusika kujipanga vizuri kupitia kitengo cha interijensia na upelelezi ili kesi zao zinapofikishwa mahakamani zisikilizwe mapema ili haki iweze kutendeka kwa wakati.

“Jipangeni sawa sawa kupitia kitengo chenu cha upelelezi na interijensia ili mkileta kesi mahakamani kila kitu kiwe kimekamilika na sisi tutazipa kipaumbele ili zisikilizwe kwa haraka,” alisisitiza

Mhe. Ngwembe alibainisha kuwa kuingilia maeneo ya Hifadhi za Taifa sanjari na kupatikana na nyara za Serikali ni miongoni mwa makosa matano ambayo yameripotiwa kwa wingi mahakamani. Alisema takwimu zinaonesha mwaka 2021 kesi 59 zilifunguliwa huku mwaka 2022 kuanzia Januari hadi Machi zaidi ya kesi 45  zilikuwa zimeripotiwa mahakamani zikihusisha ujangiri na uvamizi wa hifadhi.

“Ndio maana katika kuimarisha elimu tumewahusisha wenzetu wa Hifadhi za Taifa, Misitu na TAWA ili wawafundishe wananchi tuweze kuwafikia wengi zaidi, lengo likiwa kupunguza makosa haya ya ujangiri. Tunayo kazi ya ziada ya kuwaelimisha wananchi kwani wanaofungwa katika magereza haya ni watoto, ndugu, rafiki na jamaa zetu,” alisema.

Awali wakati akisoma taarifa fupi, Mkuu huyo wa Hifadhi aliipongeza Mahakama kwa uwepo wa mahusiano ya kikazi na Hifadhi hiyo.  Amesema changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni wanyama wadogo wadogo kuuwawa kwa kutumia silaha kama panga.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa hifadhi alibainisha kuwa ujangili wa tembo hifadhini hapo umepungua kwa kiasi kikubwa, ambapo tokea mwaka 2017 hakuna tembo aliyeuwawa. Kamishina Msaidizi Mombo aliongeza kuwa changamoto nyingine ni kesi za kugongwa wanyama ndani ya hifadhi. 

Amesema licha ya sheria kali zilizowekwa bado kumekuwa na matukio mengi ya kugongwa wanyama na watu wanaotumia barabara inayokatiza katika hifadhi. Alitoa takwimu zinazoonyesha kuwa kati ya mwaka 2014 hadi 2019 jumla ya wanyama 2,178 waligongwa na kati ya mwaka 2020 hadi 2021 wanyama zaidi ya 800 wamegongwa.

Mhe. Ngwembe alipata mwaliko wa kutembelea hifadhini hapo kujionea makundi makubwa ya wanyama mbalimbali na vitutio vya asili. Aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Sylvester Kainda, Hakimu Mkazi, Mhe. Japhet Manyama, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya, Mhe. Maua Amduni.  Mahakimu wengine ni Mhe, Salma Said, Mhe. Irene Ryatuu na Mhe. Lameck Mwamkoa.

Hifadhi za Taifa na Mahakama ni wadau ambao wamekuwa na ushirikiano wa kikazi ambapo mwezi Juni Mahakama ilitoa mwaliko kwa maafisa wa Hifadhi na Misitu kufika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kutoa elimu kwa wananchi inayohusiana na makosa ya ujangili, lengo likiwa kupunguza kesi za aina hiyo mahakamani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi kamishina Msaidizi Mathew Mombo (wa tatu kushoto) pamoja na Mahakimu walioambatana naye kutembelea hifadhini hapo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama kwenye lango la kuingilia kwenye Hifadhi ya Mikumi. Kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Japhet Manyama. Wanaofuatia kushoto kwa Jaji Mfawidhi ni Mhe.  Irene Ryatuu, Mhe. Lamek Mwamkoa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe Sylivester Kainda, Bw. Erimona Machicha, Mhe. Salma Said na Bw. Mogela.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akisaini kitabu cha wageni alipofika hifadhini hapo.
Msafara wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe ulipata nafasi ya kutembelea ujenzi wa hotel ya Mikumi Wildlife ambayo iliungua moto na kesi yake kusikilizwa na Mahakama miaka ya nyuma.
Miongoni mwa wanyama wanaopatikana katika Hifadhi ya Mikumi.

Viboko katika bwawa ndani ya  Hifadhi ya Mikumi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni