Na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Wilbert Chuma amewataka watumishi wapya wa Mahakama kuzingatia uadilifu, maadili
mema na kuepuka kufanya vitendo vinavyoweza kuwavunjia heshima kwa jamii wanayoitumikia.
Mhe. Chuma ametoa wito huo leo tarehe
18 Julai, 2022 mjini Lushoto wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi
na Wasaidizi wa Kumbukumbu walioajiriwa hivi karibuni na Mahakama ya Tanzania.
Amesema waajiriwa wapya wanatakiwa kujenga
tabia ya kujifunza na kujua utamaduni wa Mahakama (judicial culture) na kuuishi
huku wakizingatia mipaka ya kazi zao na kila mmoja akiheshimu na kulinda mipaka
ya wengine.
Mhe. Chuma amesisitiza kuwa nidhamu
ya kazi inaendana pia na kuheshimu watumishi wengine na kutumia muda wa mwajiri
ili kuifanya Mahakama iendelea kukubalika kwa jamii inayowatumikia ili kufikia
malengo na dira yake.
Amesisitiza majukumu yao kwa mujibu
wa sheria za nchi kwa ngazi mbalimbali
katika kufikia azma ya kutenda na kutoa haki kwa mujibu wa sheria na wasiwe chanzo
cha malalamiko au kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na utendaji kazi wa
baadhi yao ambao unakiuka misingi ya utu na katiba.
Aidha, Mhe. Chuma amewataka waajiriwa
hao wapya kufanya kazi kwa ushirikiano
na watumishi watakaowakuta katika maeneo ya kazi ili kuhakikisha Mahakama
inandelea kutoa huduma nzuri ya utoaji haki kwa wananchi.
Amesema ushirikiano huo utasaidia
kufanikisha jitihada zinazoendelea kuhusu uboreshaji ndani ya Mahakama ya
Tanzania, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo na usogezaji wa utoaji za haki
karibu na wananchi.
Kwa upande wa Mahakimu, Msajili Mkuu
huyo amewasihi kuzingatia maadili ambayo kimsingi yanawataka kupunguza marafiki
na kujitoa kwenye makundi ya kijamii kama vile Whatsapp, washirika wa
kibiashara na kuachana na starehe ambazo zinaweza kutia doa taswira ya
Mahakama.
Mhe. Chuma ameongeza kuwa Mahakimu lazima
watambue kuwa wao pia ni viongozi wa umma ambao wanapaswa kuhakikisha wanapokuwa
mahakamani hawavunji heshima, kuwadhalilisha watu bila kujali ni wakili,
shahidi, mshtakiwa, mtumishi wa Mahakama na hata Hakimu mwenzake.
Watumishi hao wapya watapata fursa
ya kujifunza mada zinazogusa maisha yao binafsi, mfano kujilinda na msongo wa
mawazo na kuwa na nidhamu binafsi ya matumizi ya fedha pamoja na mambo mengine.
Vilevile watafundishwa mada mahususi
zinazohusu taaluma zao ambazo ni pamoja na usikilizaji wa mashauri ya madai ya
kawaida, ndoa, jinai, talaka, mirathi, uandishi wa hukumu na utoaji wa adhabu.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi wapya na Wasaidizi wa Kumbukumbu (juu na picha mbili chini) ambao wameajiriwa hivi karibuni wakiwa katika mafunzo elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama cha Lushoto.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni