Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewataka watumishi wote wa Mahakama mkoani hapa kutoa
huduma bora ili wajitofautishe na wengine, hivyo kuwafanya wananchi waione
Mahakama ndio sehemu sahihi ya
kuikimbilia.
Mhe. Ngwembe alitoa wito huo jana tarehe 5 Julai,
2022 alipokuwa akifungua mafunzo ya namna ya kuwahudumia wateja yaliyotolewa
kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro ili kuboresha hali ya uwajibikaji
na utoaji huduma kwa wateja wanaofika mahakamani hapo.
“Ili wote tusafiri katika chombo kimoja ni muhimu
tukatambua kuwa jukumu la kutoa huduma bora kwa mteja ni la kila mmoja wetu
bila kujali cheo na wadhifa alionao, ndio maana mafunzo haya yametolewa kwa
watumishi wa ngazi zote,” alisema.
Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa mafunzo hayo
yatakuwa endelevu kwa watumishi wa Mahakama ngazi zote, hivyo ni bora kila
mmoja awe tayari kujifunza,kuelewa na kuyafanyia kazi mafundisho yote yatakayotolewa.
Mhe. Ngwembe alisisitiza kila mmoja kujifunza
matumizi ya vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana
na Mahakama ya kisasa. Aidha amewashauri wote wenye umri unaowaruhusu kurudi
shule ili kujiendeleza kielimu wafanye hivyo kwani Mahakama ya sasa ni Mahakama
ya kisasa, sio ile ya karne ya 18 au karne ya 19.
Mkufunzi wa mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Japhet Manyama alibainisha
kuwa huduma nzuri kwa mteja ndio itakayowatofautisha watumishi hao na watoa
huduma wengine, hivyo kuwavutia wananchi kuiona Mahakama kama sehemu sahihi ya kuikimbilia na sio kuikimbia.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Morogoro, Mhe. Sylvester Kahinda alisema wameitikia wito na maelekezo
ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma na uongozi mzima ngazi
ya taifa kuwataka kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa watumishi wa Mahakama,
hivyo kuamua kuanza na mafunzo ya namna ya kuwahudumia wateja.
“Tumeanza na hili tukiamini kuwa litachangia kwa
kiasi kikubwa kutatua kero za wananchi jambo lililosisitizwa hata katika mpango
mkakati wa Mahakama,” amesema.
Akitoa shukrani kwa waandaaji wa mafunzo hayo,
Msaidizi wa Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Mwanzo Kihonda, Bw. Ally Mkasi
alisema hatua hiyo imewaongezea uwezo wa namna ya kuhudumia wateja na wapo
tayari kuendana na Mahakama ya kisasa ili kumrahisishia mwananchi kupata huduma
sahihi kwa wakati.
Katika mafunzo hayo, Mahakama Kanda ya Morogoro haikuishia
kutoa elimu kwa watumishi pekee bali watoa huduma wanaofanya kazi katika jengo
la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki nao walishirikishwa ambapo kulikuwa na mwakilishi
toka kampuni ya usafi na mwakilishi toka kampuni ya ulinzi.
Sanjari na hilo, wateja pia wana darasa lao maaalumu
linalotolewa mara tatu kwa juma, lengo likiwa ni kuweka mikakati kuanzia mteja
anapofika getini mpaka anapotoka nje ya jengo baada ya kupatiwa huduma.
Mwonekano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ulipo ukumbi ambao ulitumika katika mafunzo kwa watumishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni