Jumatano, 6 Julai 2022

MAHAKAMA YA TANZANIA YAPONGEZWA KWA UTEKELEZAJI BORA MRADI WA UBORESHAJI HUDUMA

 Na Mary Gwera, Mahakama

Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) upo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama uliofadhiliwa na Benki hiyo, ambapo wameonyesha kuridhishwa na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utekelezaji bora wa Mradi.

Akizungumza katika kikao kilichohusisha Wamiliki wa maeneo ya kimkakati ndani ya Mhimili huo (SO-Owners) pamoja na Ujumbe wa Benki hiyo tarehe 05 Julai, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Msafara ambaye pia ni Afisa kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor amesema kuwa, Mahakama ya Tanzania ni moja ya Taasisi ambazo zimefanikiwa kwa kiwango cha juu cha ubora wa utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa huduma za Mahakama (Citizen Centric Project).

“Huu ni moja ya Mradi ambao una mafanikio makubwa, tunaipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hili. Kwa kipindi chote ambacho tumekuwa tukitekeleza awamu ya kwanza ya Mradi huu tumepata ushirikiano mkubwa na mafanikio yanaonekana na kila kitu kinaenda sawa,” alisema Bi. Christine.

Akizungumza katika kikao hicho, naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Benki hiyo katika utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi 2020/2021-2024/2025.

“Kwa dhati kabisa tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipa nafasi Mahakama ya Tanzania kupata mkopo wa fedha kwa ajili ya uboreshaji wa huduma zake kwa wananchi, lakini pia napenda kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuiamini Mahakama kwa awamu nyingine kwa kuongeza fedha za kuendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi tunaahidi kutoa ushirikiano zaidi,” alisema Prof. Ole Gabriel.

Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea banda la Mahakama ya Tanzania lililopo katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ 2022 yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo mbali na kutembelea maeneo mengine katika banda hilo walipata nafasi ya kuona huduma zinazotolewa na Mahakama inayotembea katika Maonesho hayo.

Mpaka sasa ujumbe huo umetembelea sehemu ya Miradi ya ujenzi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ikiwemo Mahakama ya Wilaya Kakonko, Mahakama ya Wilaya Uvinja, Mahakama ya Wilaya Buhigwe.

Maeneo mengine waliotembelea ni pamoja na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma, Mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania-Dodoma (Mradi unaotumia fedha za ndani), Mahakama ya Wilaya Gairo, Mahakama ya Wilaya Mvomero.

Ujumbe huo unaoendelea na ziara yake ndani ya Mahakama, umepanga pia kutembelea eneo la ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kibaha-Pwani, miradi ya ujenzi ya Mahakama ya Wilaya Misenyi na Kyerwa na hatimaye kuhitimisha ziara yake kwa kukagua Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 13 Julai mwaka huu.

Mpango Mkakati wa Pili wa Mahakama (2020-2025) utatekelezwa kwa kiasi kikubwa cha Dola za Kimarekani milioni 90 ikiwa ni nyongeza zaidi ya kiasi cha awamu ya kwanza ya Mradi ambayo ilikuwa Dola milioni 65 ambazo Benki ya Dunia iliikopesha Serikali ya Tanzania kwa matumizi ya kuboresha huduma ndani ya Mahakama ya Tanzania. Ongezeko la kiwango hiki litaiwezesha Mahakama kuboresha zaidi huduma zake zote zikilenga kumfikia kila mwananchi.

Afisa kutoka Benki ya Dunia, Bi. Christine Owuor (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo wakati wa mkutano wa Viongozi waandamizi wa Mahakama wa Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, jana tarehe 5 Julai, 2022 katika ukumbi wa mikutano Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam. Wengine ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Lonard Magacha (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (wa pili kulia). 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa Viongozi waandamizi wa Mahakama na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, jana tarehe 5 Julai, 2022 katika ukumbi wa mikutano Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam.


Mjumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) Waleed Malik akitoa mchango katika kikao hicho cha kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, jana tarehe 5 Julai, 2022 katika ukumbi wa mikutano Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam.

Mjumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) Clara Meghani akitoa mchango katika kikao hicho cha kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, jana tarehe 5 Julai, 2022 katika ukumbi wa mikutano Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam.


Mjumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) Roselyn Kaihula akitoa mchango katika kikao hicho cha kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, jana tarehe 5 Julai, 2022 katika ukumbi wa mikutano Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es salaam.

Viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama wakiwa kwenye kikao.



Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali waaandamizi wa Mahakama ikiwa ni pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama.


Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya huduma za Mahakama, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (wa nne kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, mara baada ya kutembela banda la Mahakama ya Tanzania katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam.

Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (World Bank Mission) uliopo nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa huduma mbalimbali za kimahakama, ukiwa ndani ya Mahakama Inayotembea wakipewa maelezo na Mkurugenzi wa Usimamizi wa mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha (mwenye kaunda suti) wakati walipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Sabasaba Jijini Dar es salaam.

(PICHA na Innocent Kansha- Mahakama) 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni