Na Faustine Kapama, Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameahidi kushughulikia
changamoto inayowakwamisha Mawakili kutoka Tanzania Visiwani kufanyakazi
Tanzania Bara baada ya kuhitimu Skuli ya Sheria Zanzibar.
Mhe.
Prof. Juma ametoa ahadi hiyo leo tarehe 5 Julai, 2022 alipokutana na Baraza la
Uongozi wa Skuli ya Sheria Zanzibar ambalo wajumbe wake walifika ofisini kwake jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha.
Ahadi
hiyo ya Jaji Mkuu inafuatia ombi liliowasilishwa kwake na Mwenyekiti wa Baraza, Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk, ambaye ni Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani
ya Tanzania kuona nanma ya kuwasaidia katika suala hilo ambalo huulizwa mara
kwa mara na wanafunzi na wadau mbalimbali wa sheria.
Jaji
Mbarouk alisema wanafunzi na wadau huwauliza ni vipi skuli hiyo
itashauliana na uongozi wa Mahakama ya Tanzania kuona namna ya kuwawezesha
wanafunzi wanaomaliza Skuli ya Zanzibar kufanya kazi Tanzania bara.
“Hivi
sasa lipo sharti la sheria kwamba Wakili kutoka nje ya Tanzania Bara lazima awe
amefanya kazi miaka mitano kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi Tanzania Bara. Sharti
hili limekuwa likiwavunja moyo wanafunzi waliopo Skuli na wanaotarajia kujiunga
katika miaka ya baadaye" alisema Jaji Mbarouk.
Akijibu
hoja hiyo, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa suala la Mawakili wa Zanzibar kuja
Tanzania Bara kufanyakazi sio jambo baya kwani hiyo ni njia mojawapo ya
kuwajengea uwezo kwa kuwa watakutana na changamoto mbalimbali za kisheria
ambazo zitawafanya wawe wazuri zaidi.
"Maombi yenu yote hasa hili sharti la Mawakili
kutoka Zanzibar waweze kuruhusiwa kufanya kazi Tanzania Bara, nadhani (jambo
hili) siyo baya, kama tunaruhusu Mawakili kutoka nje ya Tanzania kufanyakazi
kwa urahisi kwa nini tuwazuie wanaotoka Zanzibar," Jaji Mkuu alisema.
Aidha,
Prof. Juma aliuomba uongozi wa Skuli hiyo kuwajenga uwezo wanafunzi kwa kuwapa
mafunzo ya ziada nje ya taaluma yao ya sheria ikiwemo masomo ya biashara hususani
katika uchumi wa bluu ili wakikosa kazi wawe na chakufanya, na pia katika masuala
ya sayansi na teknolojia, ikiwezekana watafute ujuzi nje ya nchi kwa kuzingatia
hali ya ajira kwa sasa inatisha.
"Kuwajengea
uwezo kutawapa nafasi ya ushindani katika upatikanaji wa ajira na hasa
ikizingatiwa kwamba Zanzibar sasa ipo katika uchumi wa bluu, hivyo ni vizuri
kuangalia namna gani wanaweza kufanya kazi katika maeneo ya uwekezaji na
biashara, wakijenga uimara katika eneo hilo hata Mawakili kutoka Tanzania Bara
watakuja kujifunza Zanzibar, naona nyinyi mna nafasi kubwa zaidi," alisema
Jaji Mkuu.
Awali
akielezea historia fupi ya Skuli ya Sheria Zanzibar, Mhe. Mbarouk alisema kuwa
Skuli hiyo ilianza kazi rasmi mwaka 2021 baada ya uteuzi wa Mkuu wa Skuli na
Baraza kupitia Sheria Namba 13 ya 2019 kufuatia aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Mhe.
Dkt. Ali Mohamed Shein kuunda Kamati ya Wataalam iliyofanya utafiti wa awali wa
kuundwa kwa Skuli ya Sheria Zanzibar.
Jaji
Mbarouk alizitaja baadhi ya kazi kubwa za Skuli hiyo kwa mujibu wa sheria kama
kuwafundisha wanasheria kuwa Mawakili, kutoa elimu endelevu katika sekta ya
sheria, kutoa mafunzo ya wasaidizi wa sheria, kutoa mafunzo ya sheria kwa
mahitaji ya sekta za sheria, kufanya utafiti na ushauri elekezi na kutoa
machapisho na kusambaza ili kuinua ufahamu wa sheria.
Mwenyekiti
wa Baraza la Skuli ya Sheria Zanzibar alibainisha kuwa Skuli hiyo imefanikiwa
kutayarisha Mtaala na Mpango Kazi wa miaka mitano kupitia msaada wa fedha
kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Amesema tayari Skuli
hiyo imeingizwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23 hivyo, wametayarisha
kanuni za taaluma na nidhamu na muundo wa taasisi na utumishi.
Wajumbe
wengine walioambatana na Mwenyekiti wa Baraza katika utambulisho huo ni Makamu
Mwenyekiti wa Baraza na Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim,
Mhadhiri Mwandamizi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Mhe. Mshibe
Ali Bakari, Mkuu wa Skuli, Dkt. Ali Ahmed Uki, Naibu Mkuu wa Skuli (Utawala),
Bw. Khamis Juma Mwalim, Naibu Mkuu wa Skuli (Taaluma), Bw. Msemo Semvua Mavare
na wajumbe wa Baraza, Prof. Mohammed Makame Haji, Hanifa Ramadhani Said na Slim
Abdallah Said, ambaye ni Rais wa Jumuiya ya Mawakili Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni