Jumatatu, 4 Julai 2022

MKANDARASI AKABIDHI JENGO JIPYA LA MAHAKAMA YA WILAYA NGARA

Na Ahmed Mbilinyi Mahakama – Bukoba.

Ujenzi wa jengo jipya la kisasa la Mahakama ya Wilaya Ngara, mkoani Kagera umekamilika na tayari Mkandarasi ameshakabidhi jengo hilo kwa uongozi wa Wilaya kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za kimahakama kwa wananchi.

Hatua hiyo ni katika jitihada za kuendeleza azma ya Mahakama ya Tanzania kuboresha huduma zake kwa wananchi zikiwemo majengo kama ilivyoelezwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025.

Hivi karibuni Mkandarasi, Bw. Samweli James kutoka Kampuni ya Moladi pamoja na Mshauri Elekezi wa Mradi, Bw. Kelvin Jonson kutoka Taasisi ya Wakala wa Majengo ya Serikari (TBA) walikabidhi jengo hilo kwa uongozi wa Mahakama katika maandalizi ya hatua za awali kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Afisa Tawala kutoka Mahakama ya Wilaya Ngara Bw. Gordian Bagobweki, ambaye alipokea jengo hili amewaomba  watumishi kulitunza  kwa kuliweka safi, matumizi mazuri ya vyoo, bustani,pamoja na vifaa vya ofisi.

Katika hafla fupi ya makabidhiano hayo, uongozi wa Mahakama, watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Ngara na Waandishi wa Habari kutoka Radio Kasibante FM walipata nafasi ya kukagua jengo hili wakipngozwa na Mkandarasi.

Sambamba na hilo, kulikuwa na kikao kifupi kilichohusisha uongozi wa Mahakama, watumishi, mkandarasi, mshauri elekezi wa mradi pamoja na waandishi wa habari ambapo mshauri elekezi aliwashauri watumiaji wa jengo hilo kulipenda, kulitunza pamoja na vifaa vilivyomo ndani yake.

Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Ngara baada ya kukamilika ujenzi wake kwa asilimia 100 na kukabidhiwa kwa uongozi wa Mahakama.
Mshauri Muelekezi wa Mradi kutoka Taasisi ya Wakala wa Majengo ya Serikari (TBA), Bw. Kelvin Johson akitoa ushauri kwa watumiaji wa jengo hilo kulipenda, kulitunza pamoja na vifaa vilivyomo ndani.
Picha ya pamoja uongozi wa Mahakama, watumishi wa Mahakama wa Wilaya Ngara, Mkandarasi kutoka Kampuni ya Moladi, Mshauri Muelekezi wa Mradi kutoka TBA, na Waandishi wa Habari mara baada ya ukaguzi na makabidhiano ya jengo hilo.
Picha ya juu na chini ni muonekana wa Alama za Anuani za Makazi zikionyesha Mtaa na Alama za Uelekeo wa kuifikia Mahakama ya Wilaya ya Ngara, Mkoani Kagera.



 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni