Jumatatu, 4 Julai 2022

MOROGORO WAFURAHISHWA NA HUDUMA ZA MAHAKAMA KUU KUSOGEZWA MKOANI KWAO

Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dodoma

Wakazi wa Mkoa wa Morogoro  wameelezea furaha yao ya kusogezewa karibu huduma za Mahakama Kuu baada ya kujengwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) ambacho kimewapunguzia  gharama walizokuwa wakitumia kwenda Dar es salaam.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dodoma na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe katika kikao cha kubadishana uzoefu na Timu ya Ujumbe wa Benki ya Dunia ambayo ipo nchini kufuatilia miradi ya Mahakama ya Tanzania  iliyotekelezwa kwa mkopo nafuu wa Benki hiyo.

Alisema kabla ya ujenzi wa IJC Morogoro, wapo wakazi wa huko walikuwa wakisafiri zaidi ya kilometa 400 kutoka maeneo kama vile Malinyi na maeneno mengine kwenda Dar es salaam kwa ajili ya kufuatilia huduma za Mahakama Kuu.

Mhe. Ngwembe aliongeza kuwa wananchi hao walikuwa wakitumia zaidi ya siku nne za kwenda na kurudi kutoka Dar es salaam ili kufuatilia mashauri yao na hivyo kupunguza muda wao wa kufanya shughuli za kulazilisha mali.

Alibainisha pia kuwa wananchi hao walilazimika kutumia gharama mara mbili mbili ikiwemo kulipia nauli na nyingine za Mawakili ambazo zinaweza kuanzia laki tano hadi milioni moja.

“Ukiongea na mkazi wa Mkoa wa Mororogo anasema uwepo Mahakama Kuu kama ni muujiza ulioshuka kutoka Mbiguni ambao umekuwa msaada mkubwa kwao,”alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Jaji Mfawidhi huyo amesema wametenga saa moja mara tatu kwa wiki ya utoaji wa elimu kwa wananchi wanaokuwepo katika Kituo hicho kufuatia uwepo wa miundombinu ya kisasa ya Majengo na ile ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Alisema lengo ni kutaka kuwapelekea wananchi elimu kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya utatuzi wa migogoro ya ndoa, mirathi, migogoro ya ardhi na mengine ili kuweka mazingira ambayo yanazungumzika kirahisi ili yamalizikie nyumbani badala ya kuyaleta mahakamani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe
Mwonekano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro kwa mbele.
Picha ya juu na chini ni sehemu ya Ujumbe wa Benki ya Dunia ambayo ipo nchini kufuatilia miradi ya Mahakama ya Tanzania  iliyotekelezwa kwa mkopo nafuu wa Benki hiyo.

(Picha na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni