Na Tiganya Vincent-Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma amesema Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na Programu ya
Uboreshaji wa Huduma katika awamu ya kwanza ya utekelezaji umefanikiwa
kuimarisha miundombinu na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na
wananchi.
Amesema hivi sasa miundombinu ikiwemo ya majengo
na ile ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano imeboreshwa ndani ya Mahakama,
jambo lililowasaidia wananchi wengi kupata huduma za haki katika mazingira
rahisi na kwa gharama nafuu.
Mhe. Prof. Juma alisema hayo Jana Jijini Dodoma
alipokutana na Timu ya Benki ya Duniani iliyofika Ofisi kwake Kujitambulisha na
kuelezea juu ya kuwasili nchini kwa ajili ya kutembelea miradi iliyotekelezwa
katika awamu ya kwanza kwa ufadhili wa mkopo wa Benki hiyo wenye masharti nafuu
na maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya pili.
Alisema miradi iliyotekelezwa awamu ya kwanza
inawiana na malengo ya Benki ya Dunia ya kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa
inaboresha utoaji wa huduma za Mahakama inasaidia katika kupambana na
umaskini pamoja na kudumisha usawa wa kijinsia.
Jaji Mkuu alisema yaliyotokana na utekelezaji wa
mpango wa uboreshaji wa utoaji wa huduma za Mahakama nchini awamu umesababisha
wapokee kutoka kwa Taasisi ya Bretton Woods kwa kufikia malengo ya mradi huo.
Kiongozi wa Timu ya ujumbe wa Benki ya
Dunia Christine Owuor alisema wamewasili nchini Tanzania kwa ziara ya
kikazi ya wiki mbili ya kukagua utekelezaji miradi yenye thamani ya Dola za
Marekani milioni 65( bilioni 141 za Kitanzania ) ambazo zilikuwa ni kwa ajili
ya uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa Mahakama.
Alisema Timu hiyo imeshapitia miradi inayoendelea
katika Mkoa wa Kigoma, Tabora na Morogoro na inatarajia kuendelea katika Mkoa
wa Kagera, Dar es salaam na Arusha ili kuona utekelezaji wake.
Kiongozi huyo alisema katika miradi ambayo
wameshapitia Tanzania imefanya vizuri kiasi ambacho nchi nyingine zinatakiwa
kutembelea miradi hiyo kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kuboresha utoaji wa
huduma za Mahakama kwa wananchi.
Aidha, Bi Christine aliongeza kuwa Ujumbe
huo pia unafuatilia kuangalia maandalizi ya jinsi Tanzania ilivyojiandaa katika
utekelezaji wa awamu ya pili ya uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa Mahakama ya
Tanzania.
Serikali ya Tanzania hivi karibuni ilisaini mkataba
wa mkopo wa masharti nafuu wa jumla ya Dola za Marekani milioni 90 ( Tshs
bilioni 200) na Benki ya Dunia ili kutekeleza awamu ya pili ya Mradi wa
Uboreshaji wa Huduma za Utoaji Haki unaolenga kuboresha ufanisi na uwazi wa
upatikanaji haki kwa wananchi kwa urahisi zaidi.
Mkataba huo ulisainiwa baada ya Benki ya
Dunia baada ya kuridhishwa na utekelezaji mzuri wa awamu ya kwanza ambao ulileta
uboreshaji kadhaa katika mfumo wa Mahakama ya Tanzania katika suala la
miundombinu na utoaji wa huduma.
"Matarajio yetu ni kuona kwamba Mradi ujao
utawawezesha watu waliombali wanapata huduma za Mahakama katika mazingira ya
karibu na kwa wakati (…) tunafurahishwa na Mahakama kwa kutumia teknolojia
habari na mawasiliano wakati wa kusikiliza na kutoa uamuzi wa mashauri
mbalimbali," alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Dk Angelo Rumisha alisema katika awamu ya pili ya mradi,
Mahakama ina mpango wa kujenga Mahakama Kuu katika kila Mkoa pamoja na kuongeza
idadi ya Mahakama za Mwanzo nchini kote.
Alisema katika utekelezaji wa awamu ya kwanza
ya uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa huduma kwa Mahakama ulipelekea
Benki ya Dunia kuitunuku tuzo kufuatia mageuzi makubwa ndani ya Mahakama.
Mhe. Dk. Rumisha aliishukuru Benki ya Dunia kwa
kuendelea kuonesha imani kwa Tanzania na kuongeza awamu ya mkopo wenye masharti
nafuu ambao utaendeleza juhudi za kusogeza huduma za utoaji haki karibu na
wananchi.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni