Na Festo Sanga-Mahakama, Kigoma
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Fredrick Manyanda amewasihi
maafisa wa Mahakama katika Kanda hiyo kuwa na uelewa wa kutosha wa kazi zao
wanazozifanya wanapotekeleza jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Mhe.
Manyanda alitoa rai hiyo hivi karibuni alipokuwa akifungua mafunzo ya siku
mbili kwa maafisa hao yaliyoanza tarehe 22 Julai 2022 kuwajengea uwezo ili
kuweza kumudu utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi. Aidha aliwaasa kushiriki
kikamilifu mafunzo yanayotolewa kwa njia ya mtandao na Chuo cha Uongozi wa
Mahakama(IJA) Lushoto.
“Jifunzeni,
jisomeeni, shirikini mafunzo mbalimbali yatakayowaongezea maarifa ya kazi zenu
mkiwa kama Mahakimu,’’ alisema na kuongeza kuwa mafunzo hayo yanaongozwa na
sera ya mafunzo (Training policy 2019) ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa
Mpango Mkakati wa Mahakama ambao, pamoja na mambo mengine, umelenga kukuza
uelewa wa misingi ya taaluma ya kisheria na kuongeza ujuzi kwa watumishi wa
Mahakama.
Washiriki
wa mafunzo walijengewa uwezo katika mada za Ulinzi wa Wakimbizi, Uwepo wa Wakili
katika Mahakama za Mwanzo, Marekebisho ya hivi karibuni kwenye Sheria za Kiutaratibu,
Mahakama Mtandao, Kanuni za Maadili za Maafisa wa Mahakama na Mpango Mkakati
awamu ya pili (2020/2021-2024/2025).
Wawezeshaji
wa mafunzo hayo walikuwa ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha, Naibu Msajili Mhe. Gadiel Mariki, Mtendaji wa
Mahakama Kanda, Bw. Moses Mashaka, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kigoma, Mhe Rose Kangwa, Peter Muriyuki na Rehema Msami kutoka shirika linalohudumia
wakimbizi Kigoma(UNHCR).
Wakati
huo huo, Chama cha Majaji na Mahakimu(JMAT) Kigoma kilifanya mkutano wake ambapo,
pamoja na agenda zingine, kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa chama. Katika
uchaguzi huo, Mhe. Chiza Kabwebwe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Mhe. Venance Mwakitalu
alichaguliwa kuwa Katibu huku Mhe. Rajabu Mtuli akishika nafasi ya Mtunza
Hazina ambapo Mhe. Misana Majula alifanikiwa kuwa Mwakilishi Kamati Tendaji Taifa.
Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Fredrick Manyanda (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki na wawezeshaji wa Mafunzo. Wengine ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki (wa pili kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa (wa kwanza kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Imani Batenzi ( wa kwanza kushoto) na Bw Peter Muriyuki ( wa pili kulia) kutoka shirika linalohudumia wakimbizi(UNHCR) Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni