Jumanne, 26 Julai 2022

MKURUGENZI WA MASHTAKA AAHIDI KWENDA NA KASI YA MAHAKAMA MATUMIZI YA TEHAMA

Na. Francisca Swai – Mahakama , Musoma.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Sylvester Mwakitalu  jana tarehe 25 Julai, 2022 alitembelea Mahakama Kuu Musoma na kuahidi mageuzi makubwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya Mahakama ya Tanzania.

Akiwa katika ziara ya kikazi Mkoa wa Mara, Bw. Mwakitalu aliahidi mageuzi hayo makubwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma,  Mhe. Fahamu Mtulya ambapo ameushukuru uongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma kwa ushirikiano mzuri.

 Mkurugenzi wa Mashtaka huyo alibainisha kuwa Ofisi yake imeongezewa bajeti katika mwaka huu wa fedha, hivyo inajipanga kuongeza vifaa na kufanya manunuzi ya televisheni (screen) kubwa kwa ajili ya kuwezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (video conference).

Kadhalika, Bw. Mwakitalu alisema kuwa watanunua pia mashine kubwa ya kudurufu na kuscan (photocopier na scanner) itakayowawezesha kuendana na kasi ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA.

Mkurugenzi wa Mashtaka huyo alieleza wametangaza nafasi 82 za ajira ambazo katika watumishi hao watakaopatikana Mkoa wa Mara utafikiriwa kuongezewa kutokana na kuanzishwa kwa Mahakama mpya mbili za Wilaya ya Butiama na Rorya.

Aidha, Bw. Mwakitalu alishukuru kupata uzoefu toka kwenye uongozi wa Mahakama Kuu Musoma wa matumizi bora ya ulipaji wa fedha za mashahidi, jukumu ambalo kwa sasa litatekelezwa na Ofisi yake.

Akiongea na ugeni huo,  Mhe. Mtulya alimshukuru DPP kwa kumtembelea ili kujua hali ya kiutendaji kati ya ofisi hizo mbili. Alisema ushirikiano baina ya pande zote mbili ni mzuri na anafurahi kuona watumishi wa Ofisi ya Mashtaka wanajituma kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kwa wakati.

Alitoa mfano wa mashauri yapatayo 100 ya mauaji yaliyofunguliwa toka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kati ya mwezi Juni na Julai 2022 ambayo yamefanyiwa kazi licha ya uchache wa Mawakili wa Serikali ukilinganisha na wingi wa shughuli walizonazo katika Mkoa.

Mhe. Mtulya alisistiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na wadau wengine wa Mahakama kujitahidi kuendana na kasi ya Mahakama kwenye matumizi mazima ya TEHAMA na katika shughuli mbalimbali za Mahakama.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza ofisi za Uhamiaji kutembelea Magereza na kuwaona raia wa kigeni waliokwishamaliza kutumikia adhabu zao ili waweze kurejeshwa makwao kwa wakati.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Musoma, Mhe. Frank Mahimbali alisisitiza uwepo wa vikao vya kitaalamu (Professional meetings) kwa wapelelezi ili kukumbushwa majukumu yao itakayopelekea kufanya kazi zao kwa weledi.

Pia aliiasa Ofisi ya Mashtaka kuhakikisha mashahidi wanapatikana na kufika mahakamani kutoa ushahidi kama inavyotakiwa ikiwa ni pamoja na kuwalipa kwa wakati hasa wakati huu ambapo jukumu la ulipaji wa mashahidi limehamia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kutoka kwenye mamlaka za Mahakama.

Kutokana na kuelekea kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama za Wilaya Rorya na Butiama, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Musoma, Mhe. Frank Moshi alimwomba DPP kuweka ofisi yake katika Wilaya hizo ili mashauri yaweze kusikilizwa kwa wakati bila kusubiri Mawakili wa Serikali kutoka Musoma.

Katika ziara yake, DPP aliongozana na Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Mara, Bw.Valence Mayenga, Wakili Roosebert Nimrod kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka  Musoma, Bw. Marshal Mseja kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mara, Bw. George Mtabi kutoka Ofisi ya Uhamiaji Mara, Bw. Juma Katanga na Bw. Salimu Msemo kutoka Ofisi ya Mashtaka Dodoma.

Mkurugenzi wa Mashtaka Mhe. Sylvester Mwakitalu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Frank Mahimbali (kulia).
Picha ya pamoja ya viongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma pamoja na ugeni ulioambatana na Mkurugenzi wa Mashtaka. Mstari wa mbele katikati ni  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, wa nne kulia ni Mkurugenzi wa Mashtaka, Bw. Syliveter Mwakitalu, wa tatu kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Frank Mahimbali, wa pili kulia ni Naibu Msajili Kanda ya Musoma ,Mhe. Frank Moshi, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma, Bw. Festo Chonya na watatu kushoto ni Mkuu Ofisi ya Mashtaka – Mara Valence Myenga  na wa kwanza kushoto ni ofisa kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mara. Marsha Mseja.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni