Na Mohamed Kimungu- Mahakama, Songwe
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel jana terehe 21 Julai,
2022 alikagua ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe na Mahakama ya Wilaya
ya Songwe na kuelezea kuridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo.
Katika
ziara yake ya siku moja mkoani hapa, Mtendaji Mkuu alitembelea miradi hiyo
miwili ambapo ameridhishwa na ubora wa majengo na kuagiza kazi ya kusawazisha
eneo la nje lifanyike haraka na kwa ubora unaokubalika.
Prof.
Ole Gabriel ametoa siku sita kwa Mkandarasi, kwa maana hadi kufikia tarehe 27
Julai, 2022 kazi hiyo ya kusawazisha uwanja wa Mahakama ya Wilaya Songwe uwe
umekamilika. Amesema zoezi hilo litaenda sambamba na uwekaji samani na kupiga
vanishi vizimba vya Mahakama na kumwagiza Afisa Utumishi kupiga kambi eneo la
ujenzi na kutoa taarifa ya maendeleo kila siku kwake.
Aidha,
Mtendaji Mkuu amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Songwe kwa
kuunganisha bomba la maji katika eneo la mradi na kumwagiza Mtendaji wa
Mahakama wa Mkoa wa Songwe, Bw Sostenes Mayoka kuhakikisha Mahakama inachimba
kisima chake ndani ya miezi mitatu.
Kwa
upande wake, Msimamizi wa mradi toka Kampuni ya Moladi Construction Limited ya
Dar es salaam, Mhandisi James Jackson ameahidi kutekeleza kwa wakati kazi
iliyobaki.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni